Bodi ya Maziwa nchini (TDB) imepiga marufuku matumizi ya chupa za plastiki kwa ajili ya kuhifadhi na kuuzia maziwa.
Hayo yamesemwa na Msajili wa Bodi hiyo Dkt. George Msalya wakati wa ziara yake ya ukaguzi aliyoifanya kwa baadhi ya wafanyabiashara wa maziwa waliopo Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera leo (27.07.2021).
“Moja ya majukumu yetu kama Bodi ni kulinda afya za walaji wa maziwa na bahati mbaya chupa hizi zinatumika kuhifadhi vitu mbalimbali mara baada ya matumizi yake ya msingi hivyo huwezi kujua vitu hivyo vina athari kiasi gani kwa afya ya mlaji na ndio maana tunakataza matumizi ya chupa hizi za plastiki” Amesisitiza Dkt. Msalya.
Dkt. Msalya amewashauri wafanyabiashara wa maziwa nchini kutumia pakiti na chupa maalum zilizotengenezwa kwa ajili ya kuuzia bidhaa hiyo jambo ambalo amesema kuwa litasaidia kuhifadhi bidhaa hiyo katika mazingira salama zaidi.
“Kwa sasa tunatoa elimu badala ya kumwaga haya maziwa kwa sababu tunatambua kuwa wafanyabiashara hawa wanaitegemea shughuli hii kukidhi mahitaji yao na familia zao” Amesema Dkt. Msalya.
Akizungumzia madhara ya kiafya kwa mlaji, Mkaguzi wa maziwa kutoka Bodi hiyo Christerbel Swai amesema maziwa yanayohifadhiwa katika chupa hizo yanaweza kuganda au kuharibika kutokana na joto lililopo kwenye chupa hizo.
“Maziwa baada ya kuchemshwa yanapaswa kuhifadhiwa kwenye hali ya ubaridi tofauti na hivyo yanaweza kuharibika au kuganda jambo ambalo linaweza kumuathiri mlaji” Amesema Swai.
Swai ameongeza kuwa bidhaa hiyo haipaswi kuuzwa katika maeneo ya wazi kwa sababu inaweza kuathiriwa na uchafu unaozunguka katika maeneo yanapouzwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kikundi cha Wafanyabiashara na wasindikaji wa maziwa cha kilichopo manispaa ya Bukoba mkoani Kagera Engbert Aloyce ameishukuru bodi ya maziwa kutokana na elimu waliyopewa na kuahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na Bodi hiyo.
“Sisi tunapenda kufanya kazi zetu kwa kufuata taratibu zote tunazopewa na Serikali na kwenye hili la chupa za plastiki tupo tayari kuachana nazo ila tunaiomba serikali itusaidie kupata vifungashio vinavyotakiwa kwa gharama nafuu ambayo tunaweza kuimudu” Amesema Aloyce.
Msajili wa Bodi ya maziwa nchini, George Msalya ameambatana na wataalam mbalimbali wa Bodi hiyo kwa lengo la kukagua shughuli mbalimbali za maendeleo ya tasnia ya maziwa mkoani Kagera ili kufanya tathmini ya maeneo ambayo Bodi hiyo inahitaji kuboresha.
0 Comments