F Naibu Waziri Mary Masanja ahamasisha uwekezaji kwenye vivutio vya Utalii Nyasa | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Naibu Waziri Mary Masanja ahamasisha uwekezaji kwenye vivutio vya Utalii Nyasa

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amewataka wawekezaji nchini kuwekeza kwenye vivutio vya utalii vinavyopatikana katika Wilaya ya Nyasa ili kukuza uchumi na kuongeza ajira kwa wananchi wa eneo hilo.




Amesema hayo leo wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua maeneo ya utalii kwa lengo la kuyaboresha katika ufukwe wa Mpela, kijiji cha Kihagara Wilaya ya Nyasa leo.

“Tutaitangaza Nyasa kuhakikisha kwamba wawekezaji wanakuja Nyasa kuwekeza kwenye fukwe zetu” amesema Mhe. Mary Masanja.

Mhe. Mary Masanja amefafanua kuwa vivutio vya utalii vinavopatikana katika Wilaya ya Nyasa ni vya kipekee.


“Nyasa kuna vivutio vya kipekee kama bustani ya mawe, kuna ziwa Nyasa lenye ufukwe mzuri wenye maji safi, kuna mamba wanaoweza kuwasiliana na binadamu na kuna ngoma za asili zinazohamas” Mhe. Masanja amesema.

Ili kukuza utalii huo, Mhe. Masanja amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa kupima maeneo yote ya fukwe na kuyatangaza kwa wawekezaji ili yaanze kuingiza mapato kwa Taifa na kufaidisha wananchi wa maeneo hayo.

Aidha, Mhe. Masanja ameelekeza kuanzishwe matamasha mbalimbali yatakayovutia watalii kutembelea eneo hilo.

“Tutengeneze matamasha ambayo yatavutia wageni kutembelea hapa na tutacheza ngoma zetu za asili ili wageni waone kilichopo hapa na tutaweka viingilio ili wageni wakija waache chochote kitakachowafaidisha wenyeji” Mhe. Masanja amesema

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Mhe. Kanali Laban Thomas amesema vivutio vinavyopatikana Nyasa havipatikani sehemu yoyote duniani.

Amemshukuru Mhe. Mary Masanja kwa kuhamasisha na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo Wilaya ya Nyasa.

“Tunashukuru kwa kuendelea kuhamasisha na kuelimisha watu kuhusu utalii wa Nyasa kwa sababu watu wengi huwa wanaamini utalii ni wa wanyamapori tu” amefafanua Mhe. Thomas.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Nyasa, Mhe. Eng. Stella Manyaya amesema Nyasa iko tayari kwa ajili ya kutangaza vivutio vyake vya utalii.

Pia, Mhe. Manyanya amemshukuru Mhe. Mary Masanja kwa kutumia muda wake kutangaza vivutio vya utalii vinavyopatikana katika jimbo lake.


Ziara ya kikazi ya Mhe. Mary Masanja Wilayani Nyasa ni mwendelezo wa ziara zake za kikazi za kukagua maeneo yenye vivutio vya utalii na kuangalia namna bora ya kuyaboresha ili yaanze kutumika kuingiza mapato yatokanayo na utalii.

 

Post a Comment

0 Comments