F Tanzania na Rwanda zakubaliana kuendeleza ushirikiano katika Tehama | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Tanzania na Rwanda zakubaliana kuendeleza ushirikiano katika Tehama

 


Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Faustine Ndugulile amesema nchi za Tanzania na Rwanda zitaendelea kushirikiana na kujengeana uwezo kwenye sekta ya Tehama ili kuhakikisha zinawasaidia wananchi wa pande zote kunufaika kupitia eneo hilo.


Waziri Dk Ndugulile ameyasema hayo Julai 16 alipofanya mkutano na Waziri wa Tehama na Ubunifu wa nchi ya Rwanda, Paula Ingabire katika ofisi za Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku mbili nchini.


“Nimemkaribisha Waziri kwanza aje kuona sehemu ambayo mawasiliano yake ya nchi ya Rwanda yanapita na pili kuja kubadilishana uzoefu kwa pande zote mbili.


 “Nchini kwetu hii ni Wizara mpya (Tehama) na kwa Rwanda kuna hatua ambazo wamepiga katika maendeleo ya Tehama, lakini pia kuja kuangalia fursa zinazopatikana Tanzania na sisi kuangalia fursa hizo kwa nchi ya Rwanda,” amesema Waziri Dk Ndugulile.


Naye Waziri Ingabire akizungumza katika mkutano huo, amesema Rwanda na Tanzania zimekuwa na uhusiano wa kubadilishana teknolojia za kidigitali kwa zaidi ya miaka 10 hivyo ziara hiyo imekuja kuangalia namna ya kuboresha zaidi uhusiano huo.


Katika ziara hiyo, Waziri Ingabire aliambatana na viongozi wakuu wa taasisi zinazoratibu mawasiliano nchini Rwanda, ambapo wametembelea na kufanya majadiliano ya kimkakati na taasisi za TTCL, Kituo cha taifa cha kuhifadhi Data (Data Center) na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba, amesema ziara ya kiongozi huyo licha ya kudumisha mahusiano baina ya nchi hizo inaendelea pia kukuza kukuza biashara shirika hilo linatoa huduma za intaneti nchini Rwanda.


Aidha amebainisha kuwa wamekubaliana kuendelea kubadilishana teknolojia, mafunzo ya kujengeana uwezo, na TTCL inahakikisha inatumia fursa hiyo vizuri ili kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha mawasiliano katika ukanda wa Afrika Mashariki na Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kutimiza malengo ya Serikali.

Post a Comment

0 Comments