Ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Kagera (Kagera RVTSC) kinachojengwa nchini kwa ufadhili wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China unatarajia kukamilika ifikapo Novemba 27 mwaka huu.
Hayo
yamesemwa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omary
Kipanga akiwa ziarani mkoa wa Kagera ambapo ametembelea kuona maendeleo
ya mradi huo na kuridhishwa na hatua iliyofikiwa pamoja na kiwango cha
ujenzi.
Amesema chuo
hicho kikikamilika, kwa awamu ya kwanza kitakuwa na uwezo wa kudahili
jumla ya wanafunzi 400 wa kozi ndefu na wanafunzi 1,000 wa kozi fupi na
kwamba kitaweza kutoa huduma ya malazi kwa wanafunzi 360.
Mhe.
Kipanga amesema Serikali pia inajenga vyuo vya aina hiyo katika mikoa
ya Rukwa, Njombe, Geita na inakusudia kujenga katika mkoa wa Simiyu.
Lengo ni kuhakikisha kila mkoa unakuwa na chuo kikubwa cha umahiri
ambacho kitatoa mafunzo ya kozi maalum kulingana na mazingira na
shughuli za kiuchumi za Mkoa husika.
"Mfano
hapa Kagera kuna ziwa kwa hiyo tunatarajia chuo hiki pamoja na kozi
nyingine, kitoe kozi za uvuvi na kilimo kwa kuwa hapa mnalima kahawa,
migomba na mazao mengineyo," amesisitiza Mhe. Kipanga.
Awali,
akitoa taarifa ya mradi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Dkt. Pancras Bujulu amesema mradi huo
unahusisha ujenzi wa majengo, ununuzi wa mitambo na zana za kufundishia
na kujifunzia pamoja na uwekaji wa samani.
Amesema
mradi unatekelezwa kwa gharama ya zaidi ya Shilingi bilioni 22 na
kwamba kwa ujumla mpaka sasa utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 80.
Naye
Meneja Msaidizi wa kampuni ya Shanxi Construction Investment Group ya
China ambayo ndiyo inayotekeleza ujenzi wa mradi huo, He Tianan
ameshukuru kutembelewa na kiongozi huyo na ameahidi kukamilisha ujenzi
kwa wakati uliopangwa.
0 Comments