Tutakubaliana kuwa hali ya michezo nchini inazidi kudorora hasa ukiangalia wanafunzi wa shule za awali pamoja na upili na hata vyuo vikuu, ushiriki wa michezo sio kama miaka ya nyuma. Ingawa wanamichezo wanaweza kuumia wawapo michezoni lakini hiyo siyo sababu ya kumzuia mtu asishiriki michezo, na faida ni kubwa sana itokanayo na michezo, na kuumia michezoni kwaweza kuepukwa kwa kuchukua tahadhari.
Faida za michezo ya ushindani (mpira wa miguu, mpira wa kikapu, mbio za miguu,mbio za baiskeli,tenisi nk) ambayo hupelekea mazoezi ya viungo ziko wazi kabisa. Ni wazi pia matatizo ya kuwa na uzito mkubwa (obesity) yanaongezeka kutoka na mfumo mpya wa maisha ukilinganisha na miaka ya nyuma. Ingawa uzito wa wastani kiafya kwa wanamichezo husaidia katika ufanisi wa michezo hiyo, hiyo siyo faida pekee itokanayo na ushiriki katika michezo mara kwa mara. Miongoni mwa wanamichezo siyo rahisi kupata magonjwa ya kisukari, shinikizo kubwa la damu, na pia kujengeka katika hali ya afya njema ya viungo mbalimbali vya mwili, afya ya akili huimarika, ambapo yote hayo hupelekea kuwa na jamii ya watu wenye afya na furaha.Lakini, faida ya michezo siyo tu kujengeka kwa mwili wenye afya bora. Zifuatazo sababu chache kwa nini unatakiwa ushiriki katika michezo au kuwatia moyo watoto wetu washiriki katika michezo mbalimbali.
Sababu za kijamii.Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa, watoto na vijana wanaoshiriki katika michezo mbalimbali katika shule za awali, za upili hata vyuo vikuu, huwa hawajihusishi kwa wingi katika matumizi ya madawa ya kulevya, pombe, sigara na vitendo vya ngono ikilinganishwa na wale ambao hawajihusishi au kushiri katika michezo mbali mbali. Tafiti pia zimeonyesha wanafunzi wa kike wanaojihusisha na michezo katika shule za upili ni wacheche sana hupata mimba wakiwa katika masomo ukilinganisha na wale wasioshiriki katika michezo.
Maendeleo ya kielimu.Michezo ambayo hupelekea mazoezi ya mwili ni njia nzuri ya kujenga afya ya akili.Watoto na wanafunzi wanaoshiriki katika michezo, huwa na hamu ya kula, hupata usingizi vizuri,kinga ya mwili huimarika, hukua wakiwa wachangamfu wenye afya na miili yenye nguvu, pia afya ya akili huimarika maradufu ukilinganisha na wale wasioshiriki katika michezo. Katika utafiti mmoja uliofanyika huko Colorado Marekani, ulionyesha kuwa, wanafunzi waliokuwa washirika katika michezo, walionyesha mafanikio makubwa darasani na kuwa na matokeo yaliyotia moyo. Pia michezo itawajengea wanafunzi ujuzi katika uongozi, ujuzi ambao utawasaidia mbeleni maishani mwao.
Kazini.Utendaji na ufanisi kazini, utategemea na afya za wafanyakazi katika sehemu zao za kazi, michezo ni chombo kinachoweza kuongeza ufanisi kwa kuboresha afya za wafanyakazi. Wengi haitawaingia akilini nikiwaambia kuwa michezo inaweza kuongeza kipato cha wafanyakazi, kuwawezesha kupata cheo, kupata kazi nzuri, kuongeza ujuzi katika uongozi, kumuongezea mfanyakazi uwezo kufanya kazi kama timu na kujenga ushirikiano mzuri na wafanyakazi wengine wa kampuni moja na hata kampuni nyingine.
Mpe moyo mtoto wako kushiriki katika michezo.
Wazazi wanaweza kuwasaidia watoto wao kuwa wachangamfu na wenye afya kwa njia mbalimbali ikiwemo:
Kuongoza kwa mfano halisi, mzazi mwenyewe awe mshiriki wa michezo ili kuwa mchangamfu, mwenye nguvu na afya.
Hakikisha familia mnapotoka muwe na wakati wa michezo, au kushiriki michezo mbalimbali pamoja.
Mshawishi mwanao kutembea au kuendesha baiskeli kwa safari fupi, kuliko kutegemea kupelekwa kwa gari au kutumia usafiri wa umma.
Msapoti mwanao katika juhudi zake za kushiriki katika michezo. Ikiwezekana uwepo wakati wa mechi mbalimbali za michezo anazoshiriki, ukiwashangilia kama mshabiki wao.
Panga muda wa mtoto wa kuangalia televisheni, kompyuta au kucheza michezo mbalimbali ya kompyuta.
Wasiliana na walimu wa shule yake kuangalia uwezekano wa kumshawishi kushiriki michezo mbali mbali
0 Comments