F Lindi Mwambao chafanikiwa kuuza korosho zote katika mnada wa sita | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Lindi Mwambao chafanikiwa kuuza korosho zote katika mnada wa sita


Na Ahmad Mmow, Lindi. 

Chama kikuu cha ushirika cha Lindi Mwambao leo kimefanikiwa kuuza   korosho zake zote ghafi kupitia mnada wake wa sita kwa msimu wa 2021/2022. 

Kwamujibu wa meneja mkuu wa chama hicho, Nurdin Swallah kwenye mnada huo uliofanyika katika mtaa wa Tulieni, manispaa  ya Lindi kilo zote 1,810,557 ambazo ni sawa na tani 1,810 na kilo 557 zimenunuliwa. 

Alisema korosho hizo ghafi zilizopo katika maghala ya Hazina(Mtama), Ujenzi(Nangurukuru) na Bucco(Manispaa ya Lindi)  zimenunuliwa kwa bei ya juu ya shilingi 2,040 na bei ya chini ni shilingi 2,001. 

" Katika ghala la Buko lenye tani 306 na kilo 371 bei ya juu ni shilingi 2,040 na bei ya chini ni shilingi 2,002, ghala la Hazina lenye tani 881 na kilo 80  bei ya juu ni shilingi 2,035 na bei ya chini ni shilingi 2,021 na ghala la Nangurukuru ambalo lina tani 623 na kilo 106 bei ya juu ni shilingi 2005 na bei ya chini ni shilingi 2,001 kwa kila kilo moja," alisema Swallah. 

Meneja huyo wa Lindi Mwambao alibainisha kwamba mnada huo ulikuwa na barua 11 za kampuni zilizoomba kununua korosho hizo ambazo zilihitaji kununua tani 4,464. 

Katika hali inayodhihirisha bei ya zao hilo katika mnada huo wa sita kwa Lindi Mwambao na watisa kwa mkoa wa Lindi hazijatengemaa, alisema kwenye mnada wa tano uliofanyika katika chama cha msingi cha ushirika (AMCOS) cha Tapwa wilayani Kilwa uliotumika kunadi kilo 6,351,774 bei ya juu ilikuwa shilingi 2,210 na bei ya chini ni shilingi 2,010. 

Hadi sasa katika mkoa wa Lindi wenye vyama vikuu vya ushirika viwili (Lindi Mwambao na RUNALI) imefanyika minada tisa. Ambapo kesho Juma pili inatarajiwa kufanyika mnada wa nne kwa RUNALI na wakumi kwa mkoa wa Lindi.

Post a Comment

0 Comments