Katika kudhibiti na kusimamia kazi za udalali wa upangishaji na uuzaji wa nyumba,viwanja na mashamba, sasa madalali kuwa na vitambulisho na vyeti maalum vya kufanya kazi hiyo.
Sambamba na hilo pia madalali hao watapaswa kuwa na leseni itakayokuwa na taarifa ya mlipa kodi huku wale wa kampuni kutakiwa kuwa na mashine za kulipa kodi.
Hayo yamesemwa leo Jumatano Desemba 15,2021 na Waziri wa Ardhi,Nyumba na Makazi,William Lukuvi,alipokutana na madalali hao kutoka mikoa mbalimbali jijini humo.
Waziri Lukuvi amesema vitambulisho hivyo, dalali atapaswa kulipia Sh20,000 kwa mwaka, na vitakuwa vinapatikana katika Halmashauri zote nchini huku cheti kikiwa kinamhalalisha kufanya kazi hiyo.
"Vitambulisho hivi vitawasaidia mtambulike na kufanya kazi zenu kihalali na kuaminika kwa wapangaji na wameliki wa nyumba,viwanja na mashamba ambapo pamoja na mambo mengine serikali pia itawatambua kirahisi kwa kuwa na taarifa zenu ," amesema Lukuvi.
Amesema vitambulisho hivyo ambavyo vitakuwa na picha madalali watakuwa wanavivaa kama ilivyo kwa watumishi wa umma na kuongeza kuwa havitamfunga mtu kufanya kazi eneo jingine.
Kwa wale wenye kampuni, amesema leseni watakuwa nayo moja,ila kama ana wafanyakazi wanaoenda mtaani kila mmoja atapaswa kuwa na kitambulisho hicho.
Hata hivyo wakati sasa vitambulisho hivyo vikifanyiwa kazi amewataka kuendelea na kazi zao na kuonya kutolazimisha kuchukua kodi ya mwaka mzima kwa mpangaji na hela ya miguu na kodi ya mwezi mmoja bali amalizane na mmiliki kila kitu.
0 Comments