F Halmashauri ya Masasi DC yatoa mikopo kwa Wajasiriamali vikundi 33 | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Halmashauri ya Masasi DC yatoa mikopo kwa Wajasiriamali vikundi 33

 


Na Hamisi Nasri, Masasi.

HALMASHAURI ya wilaya ya Masasi mkoani Mtwara kupitia idara ya maendeleo ya jamii imekabidhi hundi yenye thamani ya sh.155 milioni kwa ajili ya mikopo ya asilimia 10 isiyo na riba inayotokana na fedha za mapato ya ndani ya halmashauri kwa jumla ya vikundi 33 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa lengo la kuendeleza shughuli zao za kichumi na kujikwamua na umasikini wa kipato.

 Utoaji wa mikopo huo ni mwendelezo wa utaratibu ambao halmashauri imekuwa ikifanya kila robo mwaka kwa kutoa mikopo ya aina hiyo kwa makundi ya vijana,wanawake na watu wenye ulemavu ambapo fedha hizo ni asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri.

Katika mikopo iliyotolewa na halmashauri hiyo ya wilaya ya Masasi jumla ya Pikipiki 12 aina ya TVS na SUNLG zimetolewa kwa vikundi vinne .ambavyo ni vijana bodaboda kutoka kata mbalimbali za halmashauri hiyo.

Hundi hiyo imekabidhi wilayani Masasi na mkuu wa wilaya wa hiyo ya Masasi, Claudia Kitta ambapo hafla ya makabidhiano ya hundi hiyo ilifanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo uliopo kijiji cha Mbuyuni makao makuu ya halmashauri hiyo.

Akizungumza na wanachama wa vikundi hivyo mara baada ya kukabidhi hundi hiyo mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa wanufaika wa mikopo hiyo wanatakiwa waaminifu na wakatumie mikopo waliyopata kama ilivyokusudiwa kwa lengo la kufanya shughuliza kuchumi ili waweze kujikwamua kiuchumi na kuweza kujiongeza kipato katika kumudu hali ya maisha yao.

Alisema wanufaika hao pia wanapaswa kutambua kwamba fedha hizo sio za hisani bali ni za mikopo ambayo haina riba kama ilivyo kwa mikopo inayotolewa na taasisi mbalimbali za kifedha, hivyo wakazitumie na kurejesha kwa wakati ili vikundi vingine na wao waweze kukopeshwa kwa walivyokopeshwa wao.

“Leo mmekopeshwa fedha hizi ili mkazitumie vema katika shughuli zenu za ujasiriamali hivyo tunawaombeni mzingatie kufanya marejesho kwa wakati ili na vikundi vingine pia na wao waweze kukopeshwa,’alisema Kitta  

Kwa upande wake, afisa maendeleo ya jamii halmashauri ya wilaya ya Masasi, Neema Joseph alisema halmashauri imefanikiwa kutoa mikiopo kwa makundi ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavuu ambapo jumla ya mikopo iliyotolewa ni zaidi ya sh.155 milioni kwa makundi hayo.

Alisema kuwa katika mikopo hiyo ya sh.155 milioni vikundi vya wanawake ni 20 na wamepatiwa jumla ya sh.81.5 milioni, vikundi vya vijana wao wamepatiwa jumla ya sh.70 milioni huku makundi matatu ya watu wenye ulemavu wao wamepatiwa jumla ya sh.3.5 milioni hivyo utoaji huo wa mikopo kwa halmashauri utakuwa endelevu ili kuwawezesha vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kuweza kujikwamua kiuchumi.

“Niseme tu kwamba halmashauri yetu kupitia idara ya maendeleo ya jamii itaendelea kutoa mikopo huku pia tukijikita zaidi ya katika kukusanya majeresho ya mikopo hii ili fedha zinazopatikana tuunganishe zile za mapato ya ndani kwa ajili ya kutoa kwa vikundi vingine,”alisema Joseph

 Katika mwaka wa fedha wa 2020/2021 halmashauri ilitoa jumla ya mikopo kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu jumla ya sh 191 milioni ambapo hadi sasa jumla ya fedha iliyorejeshwa ni sh.66 milioni pekee huku zaidi ya sh 100 ikiwa bado haijarejeshwa.Naye mkurugenzi wa halmashauri hiyo Apo Tindwa ametoa wito kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kumchangia fursa ya mikopo inayotolewa na halmashauri kwani halmashauri imekuwa ikitekeleza matakwa ya serikali ya kutaka kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya kusaidia makundi maalumu kuwawezesha kiuchumi kupitia shughuli zao za ujasiriamali.

Akizungumza kwa niaba ya wanufaika wenzake wa vikundi hivyo Ajira Ekoni kutoka kikundi cha wapambanaji kilichopo kijiji cha Makanyama alisema anaipongeza halmashauri kwa kuwapatia mikopo hiyo na kwamba wao katika kikundi chao wamepatiwa jumla ya sh.10 milioni na kwamba wanaahidi kujeresha marejesho kwa wakati.

Post a Comment

0 Comments