F Madarasa mapya 640 yanajengwa Mkoa wa Geita - Waziri Kairuki | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Madarasa mapya 640 yanajengwa Mkoa wa Geita - Waziri Kairuki



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Angellah Kairuki amesema Madarasa mapya 640 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 12.8 yanajengwa katika mkoa wa Geita kwa ajili ya kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza januari, 2023.

Waziri Kairuki ameyasema hayo leo tarehe 15 Oktoba 2022 wakati akimkaribisha Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kuwahutubia wananchi wa Mkoa wa Geita katika ziara yake ya kikazi ya siku moja mkoani humo.

Amesema mwezi wa tisa mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan alitoa shilingi bilioni 160 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 8,000 nchi nzima vitakavyoweza kupokea wanafunzi wa  kidato cha kwanza mwakani.

Waziri Kairuki amesema kupitia mradi wa kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP), Mkoa wa Geita umenufaika na ujenzi wa shule mpya saba ambapo kila Halmashauri imejengewa Shule mpya moja ya sekondari.

Aidha, Waziri Kairuki amesema katika mwaka wa fedha 2021/22, Rais Samia amewezesha ujenzi wa Hospitali 3 katika halmashauri za Geita Vijijini, Mbogwe na Nyang’hwale mkoani Geita.

Vile vile, amesema Rais Samia ametoa shilingi  milioni 900 kujenga Zahanati 18 katika mkoa wa Geita na ametoa Shilingi Bilioni 4.1 kumalizia Ujenzi wa vituo vya afya 13.

Wakati huo huo, Waziri Kairuki amesema Mkoa wa Geita umetengewa bajeti ya shilingi biloni 17.1 za kujenga barabara kupitia TARURA ambalo ni ongezeko la asilimia 264 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka wa fedha uliopita.

Post a Comment

0 Comments