Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye ameipongeza Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kwa kuchukua hatua za haraka katika kutatua changamoto ya uchache wa mawakala wa mbolea za ruzuku katika mkoa huo.
Ametoa pongezi hizo leo tarehe 25 Oktoba, 2022 kwa Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Dkt. Stephan Ngailo aliyewasili mkoani hapo kwa shughuli za kikazi ya siku 3 iliyolenga kufuatilia mwenendo wa uuzaji wa mbolea kwa wananchi nakutoa taarifa ya kuongezeka kwa mawakala sita huku juhudi za kuendelea kupanua wigo wa uuzaji wa mbolea kwa mawakala waliopo ukiendelea.
"Tunashukuru kwa kuona taabu tulizokuwa tunapata kufuatia uchache wa mawakala mategemeo yangu ni kwamba hata hao wachache wataangalia namna watakayofanya ili kupeleka huduma maeneo mengine ya pembezoni" Mkuu wa Mkoa Andengenye aliongeza.
Aidha, Mkuu wa Mkoa Andengenye aliwataka maafisa ugani wa mkoa huo kushiriki katika kutoa taarifa ya maeneo waliyowasajili wakulima na wapo tayari kununua mbolea ili mawakala na kampuni za mbolea ziweze kuwafikishia wananchi mbolea katika maeneo hayo.
Akizungumza katika kikao kifupi na mkuu wa mkoa Andengenye, Dkt. Stephan Ngailo amesema baada ya ofisi yake kupokea changamoto ya kuhusu uchache wa mawakala mkoani humo, ofisi yake imechukua hatua ya kuongeza mawakala pamoja na kuyataka makampuni ya uingizaji wa mbolea kupanua wigo wa usambazaji ili kuondoa kadhia hiyo kwa wananchi.
Ameeleza kuwa, ofisi yake imefanya jitihada ya kuwakutamjisha wafanyabiashara wenye mitaji na kampuni ya OCP na hivyo kuweza kuongeza jumla ya mawakala wapya sita (6) ndani ya wiki moja watakaosaidia kufikisha huduma hiyo karibu na wakulima.
Amebainisha kuwa mawakala hao wapya watauza mbolea katika wilaya za Kasulu TC mawakala wawili, Kibondo DC, Uvinza DC mawakala wawili na Kasulu DC wakala mmoja.
Akizungumzia hali ya upatikanaji wa mbolea katika Mkoa wa Kigoma, Dkt Ngailo amesema,mpaka leo maghala yaliyopo mkoani humo yana jumla ya kiasi cha tani 1454.4 za mbolea na kiasi kinachotarajia kufika ndani ya wiki hii ni tani 1492 za mbolea.
Aidha, Dkt. Ngailo amewatoa hofu ya kuwa wakulima kuwa mbolea ya ruzuku itakwisha na kuwataka wanunue mbolea kulingana na mahitaji sawasawa na hatua ya mazao yao huku akikazia kuwa mbolea zitakuwepo msimu wote wa kilimo na wakulima wataendelea kupewa huduma hiyo.
0 Comments