F Askari wa wacharuka, wakiweka mtegoni chama cha wafugaji, kamishna wa polisi aachwa Lindi aongoze operesheni. | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Askari wa wacharuka, wakiweka mtegoni chama cha wafugaji, kamishna wa polisi aachwa Lindi aongoze operesheni.

 


Na Ahmad Mmow, Nachingwea.

Katika kuhakikisha migogoro baina ya wakulima na wafugaji inakoma mkoani Lindi, mawaziri Hamad Masauni na Mashimba Ndaki wametoa maagizo mazito ambayo yanapaswa kutekelezwa na chama cha wafugaji na jeshi la polisi mkoani humu.


Mawaziri hao( Mashimba Ndaki wa mifugo na Hamad Masauni naibu mambo ya ndani) walitoa maagizo hayo jana katika kijiji cha Ngunichile, tarafa ya Lionja, wilaya ya Nachingwea mkoa wa Lindi walipozungumza na wananchi kupitia mkutano wa hadhara.


Waziri Masauni alisema vitendo vya vurughu havikubaliki na lazima jamii itii sheria. Huku akiweka wazi kwamba yanayofanywa na baadhi ya wafugaji hayakubaliki na hayavumiliki.


Masauni alisema kwamujibu wa sheria wahalifu wanatakiwa kushughulikiwa kisheria. Nakwamba serikali haipo tayari na haitakuwa tayari kuzungumza na kujadiliana na wahalifu.


Alisema baaadhi ya wafugaji wamehama kutoka kwenye maeneo yaliyotengwa na kuingia katika maeneo yasiyotengwa na hata katika vijiji ambavyo havipo kwenye mpango wa kupokea wafugaji. Hata hivyo wafugaji wameingia katika vijiji hivyo bila kufuata taratibu.


Alisema licha ya baadhi ya wafugaji kuingia katika vijiji ambavyo sio miongoni mwa vijiji vilivyokubali kupokea wafugaji, lakini pia wanatenda vitendo vya uhalifu ikiwamo vya kijinai. Hali ambayo inasababisha taharuki kwa wananchi wa vijiji hivyo. Hasa wakulima.


Waziri Masauni alisema baadhi ya wafugaji wanaiba mifugo, wanajeruhi watu na hata kuuwa. Hasa wakulima ambao wanajaribu kuzuia mazao yao yasiliwe na mifugo, hasa ng'ombe.


Kwakuzingatia hali hiyo isiyokubalika kwa wapenda amani, mshikamano, utulivu na umoja, waziri Masauni ameliagiza jeshi la polisi kuwasaka wote ambao wamesababisha vurugu, kujeruhi, kuiba mifugo na waliouwa.


Lakini pia naibu huyo mwenye dhamana ya mambo ya ndani alikwenda mbali kwakuagiza opesheni hiyo kambambe itawahusu na viongozi waliowapokea wafugaji bila kufuata taratibu.


Aidha Masauni amewataka viongozi wa chama cha wafugaji washiriki kikamilifu zoezi hilo ili wafugaji walioiba mifugo wapatikane na warejeshe mifugo waliyoiba, waliojeruhi na wanaoshukiwa kuuwa.


Alisema hicho kitakuwa  ni kipimo sahihi kama chama hicho kinastahili kuendelea kuwepo ama la. Iwapo kitashindwa kufanikisha agizo hilo hatosita kumuagiza msajili akifute chama hicho.


Katika hali inayodhihirisha naibu waziri huyo alikuwa hatanii na anataka maagizo yake yatekelezwe kikamilifu alisema atamuacha mkoani Lindi kamishna wa polisi, Hawadh Haji asimamie operesheni hiyo. Nakwamba serikali haipo tayari kufanya suluhu na wahalifu.


Kwaupande wake waziri Ndaki aliwataka wafugaji ambao wapo katika vijiji na maeneo yasiyotengwa kwa ufugaji waondoke mara moja kwa hiyari. Kwani watakaokaidi watakiona chamoto.


Waziri Ndaki alirejea kauli yake aliyotoa juzi katika kijiji cha Lineng'ene wilayani Liwale kwamba hakuna mbabe anayeweza kuishinda serikali. Huku akiwashangaa wafugaji kuvamia maeneo yasiyotengwa kwa ufugaji wakati serikali imetenga maeneo maalumu kwa ufugaji.


Alisema katika wilaya ya Nachingwea wametengewa eneo katika kijiji cha Matekwe ambacho kipo tarafa ya Kilimarondo. Akibainisha kwamba tayari kumejengwa bwawa na miundombinu mingine. Hali kadhalika katika wilaya nyingine wametengewa maeneo. Kwahiyo wafugaji waliokatika kijiji hicho na vingine ambavyo havipo kwenye orodha ya kuwapokea wafugaji lazima waondoke watake wasitake.


Aidha aliitoa wito kwa serikali ya wilaya ya Nachingwea isimamie na kuhakikisha wakulima ambao mazao yao yameliwa na kuharibiwa na mifugo wanalipwa kulingana na thamani ya mazao yao yaliyoharibiwa.


Waziri Ndaki nae alisisitiza kwamba serikali haipo tayari kujadiliana na wahalifu. Badala yake hatua za kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.


Post a Comment

0 Comments