Na Ezekiel Mtonyole – Dodoma.
Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia, Prof.Adolf Mkenda amekutana na Wamiliki wa shule
binafsi hapa nchini huku akiwataka wamiliki hao kusimamia maadili katika shule
zao na kuwataka kutoa taarifa mapema kwenye mamlaka husika wanapobaini viashiria
vya vitendo visivyo vya kimaadili.
Pia amewataka wamiliki wa shule binafsi pamoja na wadau wengine kuipitia
rasmu ya maboresho ya sera ya elimu pindi itakapotoka ili pindi itakapo
pitishwa tayari kwa utekelezaji kusiwe na malalamiko.
Akizungumza kwenye
kikao hicho Waziri Prof. Mkenda amesema
suala la maadili lazima liangalie kwa ukaribu na kufanyiwa kazi mapema
ikiwa ni pamoja na kuwafichua watu wanaofanya vitendo hivyo.
”Wamiliki simamie
malezi kwa wanafunzi wetu katika shule zenu ili kuendelea kutoa kizazi
chenye maadili na kuondokana matukio mabaya yanayoripotiwa katika baadhi ya
shule kuwa kuna mafundisho yanayotolewa ya tabia chafu.”amesema Prof.Mkenda
Ameongeza kuwa “Tupo
katika maboresho ya sera ya elimu na muda si mrefu rasmu itatoka ili wadau
waisome ni vizuri na ninyi mkaipitia kwa makini ili kama inahitaji maboresho
mengine au kuongezwa baadhi ya vitu” amesema.
Sambamba na hilo Prof.
Mkenda amewataka wamiliki wa shule kuwa makini na vitabu vinavyotolewa kama
misaada kuwa ni lazima vichunguzwe kwa umakini kabla ya kuanza kutumika katika
shule zao.
“Tunayo maadili
yetu ambayo lazima tuyalinde na kuyasimamia yasipotee, hata vitabu
vinavyotumika lazima sasa vikaguliwe kabla ya kuanza kutumika ili kuondokana na
matumizi ya vitabu ambavyo havina maadili kwa jamii yetu,”amesema.
Hata hivyo Waziri Mkenda amesema
Serikali inatambua na kuthamini mchango unaotolewa na shule binafsi katika
kuinua na kuendeleza sekta ya elimu hapa nchini.
“Niwatoe wasiwasi kuwa Serikali inatambua na inathamini mchango wenu katika maendeleo ya sekta ya elimu hapa nchini hivyo msifikirie kwamba tumewaacha nyuma hapana tunawahitaji sana muendelee kuwekeza katika Elimu yetu,”amesema Prof.Mkenda
Pia Waziri Mkenda amesema kuwa suala la wizi na uvujishaji wa mitihani ni jinai na kutangaza kuwachukulia hatua watendaji, wasimamizi, walimu na wote watakaothibitika kuhusika katika jambo hilo na kusababisha shule binafsi zipatazo 22 kufungiwa vituo vya mitihani.
“Mitihani ni gharama katika shule hizo kulikuwa na wasimamizi wa mitihani, vyombo vya ulinzi na usalama ikiwemo, watu kutoka taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa(TAKUKURU), Polisi, usalama wa Taifa, Baraza la mitihani, labda niwambie tatizo hilo la wizi wa mitihani halipo kwenye shule binafsi pekee lipo hata shule za Serikali,”amesema Mkenda.
Katika hatua nyingine Prof. Mkenda amesema Wizara itapitia suala la wingi wa tozo ambao umekuwa ukilalamikiwa na wamiliki na wadau wa shule binafsi ili kuendelea kuvumia wawekezaji wengine katika kuendesha shule.
Kwa upande wao Wamiliki wa Shule binafsi wamemuomba Prof. Mkenda katika bajeti ya Wizara ijayo kuongeza bajeti ya kuwalipa idara ya Uthibiti Ubora wa Shule wakati wanakwenda kutekeleza jukumu la kukagua shule kwani imekuwa ikiwaumiza kulipa ili waende kukaguliwa.
Pia Wamiliki hao wameomba kuondolewa kwa gharama za Mitihani kwa wanafunzi wanaosoma katika shule binafsi kwani hawana tofauti na wanafunzi wanaosoma shule za Serikali ambao wao wamefutiwa gharama za mitihani.
0 Comments