Na Ezekiel Mtonyole - Dodoma
Shirika la umeme Tanzania TANESCO limeingia makubaliano na kampuni ya ujenzi ya SINOHYDRO kwa ajili ya ujenzi wa mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa jua utakaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 174. 76 ambao hadi kukamilika kwake utaweza kuzalisha megawati 150 na kuziingiza katika gridi ya taifa.
Mradi huu mkubwa kuwahi kutokea wa kuzalisha umeme kwa kutumia jua hapa nchini na katika ukanda wa Afrika mashariki utatekelezwa kwa awamu mbili ambapo katika awamu ya kwanza zitazalishwa megawati 50 Kutoka wilaya ya Kishapu mkoani shinyanga na kuingizwa kwenye gridi ya Taifa.
Hafla ya utiaji saini
makubaliano hayo imefanyika Mei 29, 2023 mjini Dodoma ambapo ilishuhudiwa na
waziri wa Nishati Mhe. January Makamba ambapo aliipongeza TANESCO kwa hatua
iliyofikia kupatikana kwa mkandarasi na hatimae kusainiwa kwa mkataba huo ambao
utagharinu kiasi Cha shilingi bilioni 275 pindi utakapokamilika .
Mhe. Makamba amesema kuwa
serikali kwa kutambua umuhimu wa uzalishaji wa umeme kwa kutumia Nishati
jadidifu kwa Sasa WIZARA inaandaa mpango mkakati wa kuhakikisha kuwa TANESCO
inafanya upembuzi yakinifu na kuainisha maeneo ambayo yanafaa kuzalisha umeme
kwa kutumia vyanzo vya Nishati jadidifu.
“Serikali kupitia WIZARA ya
Nishati inakamilisha mpango mkakati wa uwekezaji kwenye maeneo haya kwani kwa
sasa yanapewa kipaumbele sana kwenye uzalishaji wa umeme na naiagiza TANESCO
itengeneze mwongozo unaoonyesha maeneo yote yanayofaa kwa uwekezaji kwa kutumia
Nishati jadidifu” alisema Makamba
Akizungumza juu ya mradi huo wa kuzalisha umeme kwa njia ya jua mkurugenzi mtendaji wa TANESCO Maharage Chande amesema mradi huo utatekelezwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza utazalishwa megawati 50 na awamu ya pili megawati 100 na utatekelezwa na kampuni ya SINOHYDRO CORPORATION kutoka nchini China.
Maharage amesema kusainiwa
kwa mkataba huu ni sehemu ya mpango wa mapinduzi katika kuzalisha umeme kutumia
vyanzo mbadala ukiacha vile vya maji,na gesi nchini ili kufikia lengo la kuwa
na Megawati 5000 kwenye gridi ya taifa ifikapo 2025.
Utekelezaji wa mradi huo
unatekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mkopo
uliotolewa na Shirika la maendeleo la Ufaransa (AFD) unatarajiwa kuanza mwezi
juni 2023 ambapo utachukua miezi 14 hadi kukamilika kwake.
Utiaji saini Mkataba huu
ulishuhudiwa na Waziri wa Nishati Mhe January Makamba,Naibu waziri wa Nishati
Mhe Stephen Byabato, mkuu wa mkoa wa Dodoma Mhe Rosemary Senyamule,Mkuu wa Mkoa
wa Shinyanga Christina Mndeme,Waheshimiwa wabunge viongozi waandamizi wa wizara
na menejimenti ya TANESCO waliohudhuria hafla hiyo katika ukumbi wa Morena
ulioko Mkoani Dodoma.
0 Comments