Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mwanza na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja ameongoza harambee ya kuchangia ujenzi wa nyumba ya ibada ya Kanisa la Waadventista Wasabato SDA Pasiansi kwenye Jimbo Kuu la Nyanza Kusini leo mkoani Mwanza na kupata kiasi cha shilingi milioni 95. 2 ambapo fedha taslimu zilikuwa shilingi milioni 47.3 na ahadi shilingi milioni 47.8.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Masanja amelipongeza kanisa la SDA Pasiansi kwa kuanza ujenzi wa kanisa hilo jipya ambalo ujenzi wake ulianza mwaka 2022 huku waumini wa kanisa hilo wakiwa wameshafanikiwa kuchangia shilingi milioni 56 za ujenzi.
"Serikali inatambua mchango wa kanisa hili katika sekta ya Elimu na Afya. Ujenzi wa kanisa hili ni wito na wajibu wa kila mmoja wetu" amesema Mhe. Masanja
Amesema lengo kuu la kufanya harambee hiyo ni kutafuta fedha za ujenzi wa kanisa na fedha zinazohitajika ni zaidi ya milioni 200.
Amewaomba waumini wa kanisa hilo waendelee kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuleta maendeleo na pia kuendelea kuiombea Tanzania iendelee kuwa na amani, umoja na upendo.
Naye, Mchungaji wa Kanisa la SDA Pasiansi Harun Kuyenga amesema mradi huo wa ujenzi la kanisa ulianza mwaka 2022 na unatarajia kukamilika mwaka 2024 na mara baada ya kukamilika kwake kanisa litakuwa na uwezo wa kubeba waumini 3000 ambapo kanisa la sasa lina uwezo wa kubeba waumini 800.
Ameongeza kuwa wameamua kujenga kanisa hilo jipya kutokana na ongezeko la waumini kutoka maeneo tofauti tofauti huku akisisitiza kuwa kwa sasa kiasi cha fedha shilingi milioni 200 zinahitajika ili kukamilisha ujenzi wa Kanisa hilo.
0 Comments