F Oryx Gas yagawa bure mitungi ya gesi 600 kwa vikundi vya akina mama Kigoma | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Oryx Gas yagawa bure mitungi ya gesi 600 kwa vikundi vya akina mama Kigoma


KAMAPUNI ya Gas ya Oryx Tanzania imegawa bure mitungi ya gesi ya Oryx 600 pamoja majiko yake kwa  vikundi vya akina mama katika Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma lengo likiwa ni muendelezo wa kampuni hiyo kuhimiza matumizi ya nishati safi na salama kwa kupikia.

Mitungi hiyo imekabidhiwa ushirikiano wa  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu)Profesa Joyce Ndalichako huku kampuni ya Oryx ikisisitiza malengo yao ni dhahiri kuona mabadiliko makubwa katika matumizi ya nishati safi na salama kwa ajili ya kupikia kwa jamii zote za Watanzania.

Akizungumza wakati wa kugawa mitungi hiyo kwa makundi ya wanawake hao wa Wilaya ya Kasulu Mkurugenzi Mtendaji wa Oryx Gas Tanzania Araman Bonoite  amesema mipango yao ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia inakwenda  na mpango wa Serikali wa miaka kumi wa matumizi salama ya nishati safi ya kupikia.

"Tunafahamu kuwa kundi hili la akina mama ambao kila siku wanahudumia chakula cha Watanzania wengi, wameathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na matumizi ya kuni na mkaa hivyo, kampuni ya Oryx Gas kwa kushirikiana na Waziri Ndalichako wameamua kuiunga mkono jumuiya hii ikiwa ni hamasa kwa wengine.

"Mikoa ya Kigoma na mikoa jirani imeharibiwa kwa kiasi kikubwa na ukataji miti kwa ajili ya matumizi ya nishati ya kupikia chakula, hivyo jitihada kubwa zinahitajika ili kulinda afya na kuokoa mazingira ya mkoa huu na maeneo mengine nchini, amesema.

Ameongeza kuwa Kampuni ya Oryx inawekeza katika siku zijazo kwa kutekeleza mipango ya kukabiliana na kaboni kupitia elimu ya upishi safi, uchangiaji wa vifaa vya kuanzisha LPG bila malipo kwa baadhi ya mikoa, uhamasishaji wa matumizi ya gesi ya kupikia majumbani  kupitia uuzaji mkubwa wa mitungi ya gesi kwa bei nafuu.

Aidha  mafunzo kwa wingi kwa matumizi salama ya LPG na kadhalika, juhudi zinazolenga kuhakikisha Watanzania walio wengi wanapitisha hatua kwa hatua suluhisho la nishati safi ya kupikia kama ilivyoagizwa na Mheshimiwa rais Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Benoite amesema Rais Dk.Samia ameweka lengo la Watanzania kutumia nishati safi, ikiwa ni pamoja na LPG, kuwa angalau asilimia 80 ya watu wote ifikapo mwaka 2032. Kampuni ya Oryx Gas Tanzania inajivunia kuunga mkono maono yake katika kutoa nishati safi ya kupikia kwa Watanzania wengi.

Kwa upande wake Waziri wa  Nchi , Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Profesa Joyce Ndalichako kwa kushirikiana na Oryx Gas wamegawa mitungi hiyo kwa vikindi vya wanawake wa Wilaya ya Kasulu  lengo ni kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Waziri Ndalichako ambaye pia  ni Mbunge wa Jimbo la Kasulu Mjini amesema mitungi hiyo inakwenda kuleta auheni kwa makundi ya wanawake kwani wataachana na matumizi ya kuni na mkaa na kutumia nishati safi ya kupikia ambayo ni gesi ya Oryx.

"Kugawa mitungi hii kwa wananchi wetu ni sehemu ya jitihada za kuunga mkono juhudi za Rais Dk .Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa akihamasisha utunzaji wa mazingira kwa kutoharibu misitu yetu kwa kukata miti kwa ajili ya kupata kuni na mkaa.Hivyo niendelee kuwaomba wananchi tutunze mazingira."

Aidha Waziri Ndalichako amesema kuwa matumizi ya kuni na mkaa yamekuwa na athari kubwa za kiafya hivyo ni vema wananchi wakatumia nishati safi ya kupikia ili kuhakikisha afya za wananchi zinakuwa salamba.

Pia ametumia nafasi hiyo kueleza kuwa yeye amekuwa akitumia gesi ya Oryx kwa muda mrefu na ndio ameona ni vema wananchi wake wakapata mitungi hiyo ili kuwa kuachana na kutumia kuni na mkaa.

Pamoja na hayo , Waziri Ndalichako ameiomba Kampuni ya Oryx Gas kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya nishati ya gesi ya kupikia ili kuhakikisha wananchi wanakuwa salama wakati wote.

Post a Comment

0 Comments