Na Mwandishi wetu- DODOMA
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama amezindua Chumba cha Ufuatiliaji wa Mwenendo wa Majanga na Tahadhari ya Mapema (Situation Room for Mult-Hazard Monitoring and Early Warning) katika Kituo cha Taifa cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura.
Mhe. Jenista amefanya uzinduzi huo tarehe 14 Juni 2024 Jijini Dodoma ambapo alisema uanzishwaji wa chumba hicho muhimu cha ufuatiliaji wa majanga na tahadhari ya mapema umefanikiwa kutokana na mradi ulioanzishwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupunguza Madhara ya Maafa katika Kanda ya Afrika na kufadhiliwa na Serikali ya Nchi ya Italia kupitia Shirika la Maendeleo la Italia (Italian Agency for Development Cooperation) ambapo Taasisi ya CIMA Research Foundation ya Italia imesadia kutoa utaalam wa utekelezaji wa shughuli zote.
Aliongeza kuwa Katika kuhakikisha nchi inakuwa stahimilivu dhidi ya maafa, Serikali imeweka utaratibu mzuri wa kushughulikia masuala ya maafa kwa kuzingatia Sera ya Taifa ya Menejimenti ya Maafa ya mwaka 2004 na Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 6 ya mwaka 2022, Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi 2020-2025 Ibara ya 107 pamoja na miongozo mbalimbali ya kitaifa, kikanda na kimataifa ya utekelezaji wa hatua za usimamizi wa maafa.
“Serikali kwa kuzingatia Sheria ya Usimamizi wa Maafa na. 6 ya mwaka 2022 Kifungu cha 5 imeanzisha Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura katika ngazi ya Taifa ambacho kimeunganishwa na vituo vya kisekta kikiwa kimepewa jukumu la kisheria la kufuatilia mwenendo wa majanga, kupokea na kuchambua taarifa za tahadhari na dharura kwa ajili ya usimamizi wa maafa nchini,” Alisema Mhe. Jenista.
Vile vile alieleza kwamba kupitia majanga mbalimbali yaliyotokea nchini na athari zilizotokea, Serikali imeona umuhimu wa kuendelea kuimarisha mifumo ya tahadhari za awali na ufuatiliaji wa majanga kwa kuanzisha chumba chenye vifaa na mifumo ya kisasa kwa ajili ufuatiliaji wa mwenendo wa majanga na uchukuaji wa hatua za mapema.
“Tuendelee kuhakikisha juhudi zinazochukuliwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika kuimarisha uchumi na huduma za kijamii katika ujenzi wa Taifa letu zinakuwa stahimilivu dhidi ya maafa,” Alipongeza Mhe. Jenista.
Aidha alitoa wito kwa wataalam wote waliopangiwa na watakaopangiwa kufanya kazi katika chumba hicho kuhakikisha kuwa shughuli zilizopangwa kufanyika zinatekelezwa kwa ufanisi na kunakuwa na mwendelezo ili kuhakikisha taarifa za tahadhari za mapema zinawafikia walengwa kwa wakati hasa wanajamii na taasisi mbalimbali kwa ajili ya kuchukua hatua za haraka za kuzuia na kupunguza madhara ya majanga.
“Uwepo wa chumba hiki uwe ni fursa kwa wadau wote katika kuboresha hatua mbalimbali za kuzuia, kujiandaa, kukabiliana na maafa na kurejesha hali baada ya maafa kutokea katika maeneo yote na hatua mbalimbali za usimamizi wa maafa zinazochukuliwa na kila mmoja wenu zinachangia katika juhudi zake katika kuongoza na kusimamia utekelezaji wa mipango ya Serikali kwa manufaa makubwa kwa wananchi na tija iliyokusudiwa,”Alihimiza Mhe. Jenista.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi aliyataja majukumu yatakayotekelezwa kupitia chumba hicho kuwa ni pamoja na kufanya ufuatiliaji wa uwezekano wa kutokea kwa majanga kwa kutumia mifumo ya kiteknolojia ya kijiografia na haidrolojia iliyopo ikiwemo jukwaa la kielektroniki la MyDEWETRA.
“...hii itasaidia kufuatilia mwenendo wa janga lililotabiriwa na kufanya uchambuzi wa kiwango cha madhara kwa jamii, miundombinu na mazingira, kuandaa taarifa za tahadhari ya mapema na hatua za kuchukua ili kuzuia, kujiandaa na kukabili janga, kuandaa taarifa ya mwenendo wa tukio (situation report) na kusambaza wadau mbalimbali kwa ajili ya kusaidia uratibu na utekelezaji wa shughuli za kukabili na kurejesha hali,” Alieleza Dkt. Yonazi.
Naye Naibu Katibu Mkuu aliyemuwakilisha Katibu Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupunguza Hatari za Maafa (UNDRR) Marco Riccardo Rusconi ameeleza kuwa uzinduzi huo utasaidia kushirikiana na vituo vya kikanda na kimataifa vinavyosimamiwa na Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika na Jumuiya ya Maendeleo katika Pembe ya Afrika ili kuboresha udhibiti wa maafa yanayovuka mipaka.
Vilevile Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la Italia (Italian Agency for Development Cooperation -AICS) Prof. Eng. Luca Ferraris amesema uanzishwaji wa Chumba hicho umezingatia hatua za kuchukuliwa na kila sekta zinazohusika katika ufuatiliaji wa mwenendo wa majanga na utoaji wa tahadhari ya mapema ili kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na majanga yanayoweza kutokea kwa kuzingatia uwajibikaji wa pamoja.
0 Comments