Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Bw. Charles Makongoro Nyerere, amewataka watoa huduma ndogondogo za fedha Mkoani mwake wasajili huduma zao za kifedha kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya Mwaka 2018, na kuwaelekeza watoe elimu kwa wateja wao kabla ya kuwakopesha.
Bw. Charles Makongoro Nyerere ametoa maagizo hayo wakati wa kikao na Waandishi wa Habari katika Ukumbi Mdogo wa Mikutano wa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Wilaya ya Sumbawanga Mjini.
“Ndugu wanahabari; watoa huduma ndogo za fedha ni watu muhimu katika mkoa wetu wa Rukwa na Taifa kwa ujumla. Pamoja na umuhimu huo naagiza kuwa watoa huduma ndogondogo za fedha wote mkoani Rukwa wasajiliwe kwa mujibu wa sheria” Alisema Bw. Makongoro.
Bw. Makongoro alisema kuwa sambamba na zoezi la kusajili vikundi vidogovidogo vya huduma ndogo za fedha, ni vyema pia kwa watoa mikopo kutoa elimu kwa wanaowakopesha na kuwapa muda wa kuelewa mikataba kabla ya kuwapa mkopo.
“Mtoa huduma za kifedha toa elimu kwa yule unayetaka kumkopesha kuhusu huduma yako kabla ya kumkopesha. Na hili liende sambamba na wanaokopeshwa kupewa muda wa kutosha kusoma mikataba yao na kuielewa vizuri kabla ya kumkopesha, usimshtukize ule mkataba mpe muda ausome auelewe ndio umkopeshe.” Alisisitiza Bw. Makongoro.
Vile vile alitoa rai kwa Wakuu wa Wilaya wote wa Mkoa wa Rukwa kuwa wahakikishe wanasimamia maelekezo yake kuanzia ngazi ya Vijiji, Kata, Tarafa pamoja na Halmashauri zote.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Bw. Charles Makongoro Nyerere, alihitimisha kwa kuwaomba wananchi wote wa Mkoa wa Rukwa kutoa ushirikiano ili kuwabaini wale wote wanaotoa huduma za fedha kinyume na utaratibu wa kisheria ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Aidha, aliwashukuru wataalam kutoka Wizara ya Fedha kwa kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa mkoa wake katika Wilaya na Halmashauri zake zote.
0 Comments