FCC yabainisha madhara ya bidhaa bandia, yatoa rai kwa wananchi


WATANZANIA wametakiwa kuacha mara moja matumizi ya bidhaa bandia na badala yake kuhakikisha kuwa wanatumia bidhaa halisi hali itakayosaidia kuchochea uwekezaji, kukuza fursa za ajira na hatimaye kuchagiza ukuaji wa uchumi wao na taifa kwa ujumla

Kauli hiyo imetolewa leo Julai 17, 2024 jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC) William Erio wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea kilele cha wiki ya kudhibiti bidhaa bandia duniani ambayo huadhimishwa kati ya mwezi Juni na Julai kila mwaka.

''Kati ya asilimia 2.5 na 3.5 ya biashara zinayofanyika ulimwenguni zinahusisha bidhaa bandia ambapo amebainisha baadhi ya madhara ya bidhaa hizo kuwa ni kutopata thamani halisi ya fedha pamoja na madhara mbalimbali ya kiafya kwa watumiaji'' amesema Bwa. Erio

Pia amewataka wafanyabiashara nchini kuacha kuagiza ama kuuza bidhaa bandia kwani kwa kufanya hivyo wanashusha ushindani wa kibiashara sambamba na kupoteza mapato ya serikali hivyo tume imeendelea kutoa elimu kwa umma kuhusiana na madhara hayo.

Hivyo, Kilele cha maadhimisho hayo yaliyobebwa na Kauli mbiu isemayo “Kudumisha uhalisia kwa kulinda ubunifu kwa maendeleo ya kiuchumi nchini” kinatarajiwa kuwa julai 18 katika ukumbi wa mikutano ya mlimani city jijini dar es salaam.




 

Post a Comment

0 Comments