KAPINGA: Taasisi zinazotoa huduma za kijamii kuunganishwa Umeme


Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema kuwa Taasisi zote zinazotoa huduma za kijamii kama shule na vituo vya afya pamoja na nyumba za ibada zitafikishiwa umeme.

Naibu Waziri Kapinga ameyasema hayo  Julai 22, 2024 wakati akiwasha umeme katika Shule ya Sekondari Nyasa iliyoko katika Kijiji cha Chimate wilayani Nyasa, Mkoa wa Ruvuma. 


“Sisi kama Wizara ya Nishati ni kuhakikisha tunaongeza tija katika taasisi hizi zinazotoa huduma kwa kufikisha umeme. Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan anahangaika usiku na mchana kutafuta fedha za kuboresha maisha ya Watanzania kila siku na kazi yetu kubwa ni kuhakikisha taasisi na maeneo yote yenye umuhimu yanafikiwa na umeme”amesema.

Aidha amesema Shirika la Umeme nchini (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wamejidhatiti katika maeneo ambayo kuna taasisi za kijamii kama shule, vituo vya afya, makanisa na misikiti kwa kuhakikisha vinafikiwa na umeme ili kuboresha huduma za kijamii katika Taifa letu,” amesema Kapinga.


Awali akitoa taarifa ya utekelezaji Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa REA, Eng. Robert Dulle amesema kuwa gharama za kufikisha umeme katika kijiji hicho ni shilingi Milioni 286.

Eng. Dulle ameongeza kuwa Mkoa wa Ruvuma unajumla ya Vijiji 554 na mpaka kufikia Julai 2024, vijiji 542 sawa na asilimia 97.8 vimepata huduma ya umeme kupitia miradi inayotekelezwa na REA huku akihamasisha wananchin kuchangamkia fursa za uwepo wa umeme vijijini kufanya shughuli za kiuchumi zitakazoboresha maisha yao.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Nyasa, Mwalimu John Ndelwa ameipongeza REA kwa kufikisha umeme shuleni hapo na kuahidi kuwa watatumia fursa ya umeme huo kuwafundisha wanafunzi masomo ya jioni na hivyo kuongeza ufaulu.

Ameongeza kuwa uwepo wa umeme utawawezesha kuwa na mitihani mingi ya majaribio kwa kuwa watakuwa na uwezo wa kuchapa mitihani wenyewe shuleni tofauti na awali ambapo walikuwa wanalazimika kutumia gharama kubwa kwenda kuchapisha katika steshenari.
 
Imeandikwa na Daudi Manongi na Iddi Mwema-Nyasa

Post a Comment

0 Comments