Kiongozi wa Mwenge Kitaifa ataka wenye mahitaji wasaidiwe


Na John Walter -Simanjiro

Jamii imeaswa kutoa msaada kwa watu wenye mahitaji maalumu wakiwepo watoto wanaoishi katika mazingira magumu ili kusaidia kukidhi mahitaji yao ya msingi.

Wito huo umetolewa na kiongozi wa mbio za mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2024 Godfrey Mnzava  mara baada ya kutembelea makao ya watoto Light in Africa  kinachowalea watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi wilaya ya Simanjiro.

"Tusiwanyanyase wala kuwanyanyapaa kwa namna yoyote ile wala kuwaficha watoto wenye mahitaji maalum, kwani serikali imeweka mazingira rafiki kwa ajili yao, hakuna kinachoshindikana chini ya jua ndo maana zipo zana wezeshi " alisema Mnzava

Amesema kuwasaidia Watoto hao ni baraka na kwamba  wanapaswa kupata huduma zote zikiwemo elimu,afya kama watoto wengine.

Kiongozi huyo amekabidhi msaada wa shilingi milioni mbili katika kituo hicho zilizotokana na michango ya mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2024 wilayani Simanjiro.

Shirika la Light in Africa lina jumla ya nyumba tano, watoto 152 ambapo kati yao wa kiume ni 75 na wa kike 77, wenye ulemavu ni 51.

Shirika hilo limefanikiwa kuwapatia Watoto huduma muhimu za malazi,mavazi,chakula, matibabu,kulipia gharama za elimu ya Msingi,sekondari na vyuo.

Post a Comment

0 Comments