Mpunga awapa matumaini wakulima.



Na Ahmad Mmow, Nachingwea. 


Katika kuhakikisha wakulima ambao wengi wao ni wanaushirika wanaondokana na changamoto zinazo sababishwa na ushindani wa kibiashara baina ya taasisi za fedha. Imeelezwa kwamba kuna mpango wa kuanzishwa benki ya ushirika.


Hayo yalielezwa juzi tarehe 14.07.2024 na mwenyekiti wa chama kikuu cha ushirika cha RUNALI, Audax Audax Mpunga kijijini Nambilanje,wilaya ya Ruangwa. 


Mpunga ambae aliyasema hayo wakati anafunga mkutano wa mnada wa tano wa ufuta  kwa chama hicho kwa msimu wa 2024, alisema licha ya benki kupata faida kupitia ushirika lakini kumekuwa na changamoto zinazotokana na ushindani wa kibiashara baina ya benki na benki na taasisi nyingine za fedha.


Alisema ushindani huo kwa kiasi kikubwa unachangia kuchelewesha malipo ya fedha za wakulima ambao wameuza mazao yao ya  kilimo kupitia mfumo rasmi.


Kwakuzingatia ukweli huo mwenyekiti huyo wa  RUNALI  alisema muda si mrefu wanaushirika watanufaika na benki ya ushirika. Kwani ushirika utamiliki asilimia 51 ya hisa za benki hiyo. Huku kipaumbele kitakuwa kuwahudumia wanaushirika.


Mpunga aliweka wazi kwamba upo uwezekano mkubwa wa benki hiyo kufunguliwa na kuanza kufanya kazi mwezi Septemba mwaka huu wa 2024.


" Kwabahati nzuri miongoni mwa matawi matatu ya awali ya benki hiyo, moja litakuwa Mtwara. Kwahiyo wakulima  changamoto hii inaweza kupungua kama sio kwisha kabisa," alisema Mpunga.


Aidha Mpunga alisema kuanzishwa na kuanza kutoa huduma benki hiyo  kutakuwa kama kipimo. Kwani itajukikana kama changamoto ya ucheleweshaji malipo ya wakulima na nyingine zinasababishwa na wana ushirika ama wadau wengine.


Katika mnada huo wakulima walikubali kuuza ufuta wao wenye jumla ya kilo 2,894,674 kwa bei ya juu ya shilingi  3,690 na bei ya chini shilingi 3,590 kwa kila kilo moja.

Post a Comment

0 Comments