Mwenge wa uhuru wazindua mradi wa maji Magara.


Na John Walter-Babati 


Mwenge wa uhuru umezindua mradi wa maji uliotekelezwa na wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini-RUWASA uliopo kijiji cha Magara Halmashauri ya Wilaya ya Babati mkoani Manyara uliotumia shilingi Milioni 801 hadi kukamilika.


Akisoma taarifa ya Mradi huo kwa Kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru Godfrey Mnzava, Meneja wa RUWASA wilaya ya Babati, Mhandisi Felix Mollel amesema utahudumia watu wapatao 5,137.


Chanzo cha mradi huo wa maji ni mto Magara ambapo mtandao wa mabomba ni kilomita 20.7.


Mkuu wa wilaya ya Babati, Lazaro Twange ameishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili mradi huo mkubwa.



Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kwa mwaka 2024, Godfrey Mnzava  amewapongeza RUWASA kwa kutimiza adhma ya serikaki ya kumpunguzia mwananchi adha ya kutembea umbali mrefu kufuata maji.


Hata hivyo baada ya Mwenge wa uhuru kuridhia kuzindua mradi huo wa maji wa kijiji cha Magara ameagiza kibao cha uzinduzi  kihamishwe kiwekwe kwenye tenki mlimani badala ya kwenye kituo cha kuchotea maji.


Nao Wananchi wa kijiji cha Magara wamemshukuru serikali kwa kuwapatia mradi huo wa maji kwani umekuwa mkombozi kwao. 


Kaulimbiu ya Mwenge wa uhuru kwa mwaka 2024  "Tunza mazingira na shiriki uchaguzi wa serikali za mitaa kwa ujenzi wa Taifa endelevu".

Post a Comment

0 Comments