RUNALI chauza kilo 2,894,674 za ufuta katika mnada wa tano.



Na Ahmad Mmow,  


Chama kikuu cha ushirika cha RUNALI leo tarehe 14.07.2024 katika mnada wa tano kwa  mwaka 2024  uliofanyika katika kijiji cha Nambilanje, wilaya ya Ruangwa kimefanikiwa kuuza kilo 2,894,674 za ufuta.


Kwa mujibu wa  afisa uendeshaji biashara wa soko la bidhaa Tanzania(TMX), Mahama Kadikilo ufuta huo ulinunuliwa kwa bei ya juu ya shilingi 3,690 na bei ya chini shilingi 3,590 kwa kila kilo moja.


Katika mnada huo ambao ufuta ulinadishwa kwa njia ya mtanda(kidigitali) katika ghala la GPZA bei ya juu na chini ilikuwa shilingi 3,620, ghala Export Trading bei ya juu na chini shilingi 3,600, ghala Hassan Mpako bei ya juu shilingi 3,600 na bei ya chini 3,590, ghala la Lipande bei ya juu shilingi 3,670 na bei ya chini shilingi 3,630, ghala Nachingwea DC bei ya juu na chini shilingi 3,69, ghala la RUNALI bei ya juu na chini ni shilingi 3,690 na katika ghala Umoja bei ya juu shilingi 3,630 na bei ya chini ni shilingi 3,620.


Akizungumza baada ya wakulima walioshiriki katika mnada huo kukubali kuuza kwa bei hizo, mwenyekiti wa RUNALI, Audax Mpunga aliwataka viongozi na watendaji wa vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS) waharakishe 

kuandaa malipo. Akiweka wazi kwamba RUNALI kimekuwa kikikamilisha maandalizi kwa wakati. Kwani wakulima wanahitaji kulipwa kwa wakati.


Aidha Mpunga alitoa wito kwa taasisi za fedha, hasa benki ziharakishe kuandaa malipo ya wakulima mara baada ya wanunuzi kuingiza fedha za malipo kwenye benki hizo.


Alibainisha kwamba mchakato wa malipo ya wakulima mchakato wake unahusisha wadau wengi, ikiwemmo benki. Kwahiyo hata mdau mmoja asipotimiza wajibu wake kwa wakati ni chanzo na sababu ya kukwamisha na kuchelewesha malipo ya wakulima.


Mnada huo ambao ni watano kwa chama cha RUNALI ni kati ya minada kumi na moja ambayo imefanyika katika msimu wa 2024 katika mkoa wa Lindi. Kwani minada sita imefanywa na chama kikuu cha Lindi Mwambao.

Post a Comment

0 Comments