Shilingi 100 ya tozo ya mafuta yajenga daraja Kiteto

 

Na John -Walter- Kiteto 

Zaidi ya shilingi Millioni 146 za Tozo ya shilingi 100 ya mafuta ya dizeli na Petrol kutoka serikali kuu zimejenga daraja la Partimbo barabara ya Kibaya -Mbeli na  kuwaondoa wananchi adha waliyokuwa wanakutana nayo pindi mvua zinaponyesha.

Akizindua daraja hilo Kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru Kitaifa Godfrey Mnzava amewapongeza TARURA kwa kusimamia vyema mradi huo kukamilika kwa wakati na kwa ubora.

Ujenzi wa daraja hilo ulianza septemba ,2023 ambao umetekelezwa kwa kujenga Kingo,tuta la barabara kuzuia mmomonyoko wa udongo na kupanda miti ili kurejesha uoto wa awali.

Daraja hilo litakalowanufaisha wananchi 53,347 limejengwa kwa teknolojia ya mawe ambayo inatajwa kuwa ya gharama nafuu zaidi hivyo kuisaidia serikali kuokoa fedha kwani endapo lingejengwa kwa zege lingetumia shilingi Milioni 300.

Taarifa ya mkuu wa wilaya ya Kiteto Remidius  Mwema imesema kukamilika kwa barabara hiyo kunachochea maendeleo ya wananchi wa maeneo hayo ambao wamekuwa wakipata adha kubwa ya barabara hususani wakati wa mvua ikiwemo kushindwa kusafirisha bidhaa mbalimbali kupeleka maeneo mengine.


Post a Comment

0 Comments