Taasisi za fedha zanyooshewa kidole kuchangia ucheleweshaji wa malipo ya wakulima.

 


Na Ahmad Mmow,  Nachingwea.


Ushindani wa biashara baina ya taasisi za fedha, hasa benki umetajwa kuchangia kuchelewesha malipo ya wakulima wa ufuta mkoani Lindi.


Akizungumza wakati wa mnada wa tano wa ufuta kwa mwaka 2024 kwa chama kikuu  cha ushirika cha RUNALI uliofanyika jana kijijini  Nambilanje, wilaya ya Ruangwa. Makamo mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Ruangwa, Mikdad Mbute ambae alizungumza kwaniaba ya  wenyeviti wa halmashauri za wilaya za Ruangwa, Liwale na Nachingwea alisema ushindani wa kibiashara baina ya benki unachangia kuchelewesha malipo ya wakulima wa ufuta ambao wanakuwa wameuza ufuta wao.


Alisema kuchelewa kulipwa fedha wakulima kunasababishwa na mambo mengi. Hata  hivyo ushindani wa kibiashara baina ya  benki una mchango mkubwa wa kukwamisha na kuchelewesha malipo ya baadhi ya wakulima wa ufuta na hata mazao mengine ambayo mfumo wake wa malipo unafanana na malipo ya ufuta.


Aliweka wazi kwamba baadhi ya wakulima ambao vyama vyao vya msingi vinafanyakazi na benki tofauti na ambazo wao wamefungua akaunti zao ni waathirika wa ushindani huo. Kwani wanazungushwa na kucheleweshewa malipo. Huku wakitakiwa kufungua akaunti kwenye benki ambazo vyama vyao vya msingi vya ushirika(AMCOS) zinafanya kazi na benki hizo.


" Tabia hiyo inasababisha hasara na usumbufu kwa wakulima. Kwasababu wanalazimika kufungua akaunti nyingine. Na wakifungua tu mzigo unaingia muda huo huo," Mbute alisisitiza.


Alitoa wito kwa taasisi hizo za fedha   ziwahudumie wakulima bila kuwahusisha katika ushindani. Kwani wakulima hawahusiki na hawana masilahi na ushindani wao. Huku akisisitiza kwamba ushindani usiwe sababu ya kuwa umiza wakulima bali wanufaike nao kwa kupewa huduma bora, nzuri na haraka.


Mbali na hayo Mbute alitoa wito kwa serikali kuangalia upya na kufuatilia mfumo na mwenendo wa usajili wa wakulima wa korosho na mgao wa viuatilifu na  pembejeo.


Amesema wakulima wengi watashindwa kupata viuatilifu na pembejeo zinazotolewa na serikali. Kwani hawajasajiliwa kutokana na sababu mbalimbali.



Kutokana na hali hiyo wakulima hao hawatapata viuatilifu na pembejeo. Kwahiyo kuna uwezekano wa viuatilifu na pembejeo kubaki maghalani wakati wakulima wengi hawajapata.


Alitoa wito kwa serikali kutafuta njia ya kuwafanya wakulima hao wapate viatilifu na pembejeo.


Nae mwenyekiti wa chama kikuu cha RUNALI,  Audax Mpunga alisema usumbufu wa benki kwa wakulima hauna muda mrefu utakwisha. Kwani serikali ina mpango wa kuanzisha benki ya ushirika ambayo walengwa wakubwa wa huduma zake ni wana ushirika.

Post a Comment

0 Comments