TMX lawapongeza wakulima wa ufuta wa mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma.

 


Na Ahmad Mmow, Nachingwea. 


Soko la bidhaa Tanzania (Tanzania  Mercantile Exchange/TMX) limewapongeza wakulima wa ufuta wa mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma kwa kudhibiti, kulinda na kuhifadhi ubora wa zao hilo.


Jana akizungumza na wakulima wa kata ya Nambilanje, wilaya ya Ruangwa mkoa wa Lindi  walioshiriki mnada wa ufuta uliofanyika katika kijiji cha Nambilanje afisa uendeshaji biashara wa TMX, Mahama Kadikilo alisema wakulima wa mikoa hiyo wanasitahili pongezi kwa kutunza, kuhifadhi na kulinda ubora wa ufuta. Hali ambayo inachangia wanunuzi kujitokeza kwa wingi kununua ufuta katika mikoa hiyo kutokana na ubora wake.


Alisema kutokana na wakulima kuandaa vizuri ufuta wao ndio sababu ya kila mnada kuvutia wanunuzi katika kila ghala. Kwani wanunuzi hao wana uhakika wa ubora wa ufuta watakao nunua.


" Mimi niwapongeze wakulima wa ufuta wa mikoa hii ya Kusini. Kwakweli mnasitahili kupongezwa. Wafanyabiashara wanapata nafuu ya gharama wanaponunua ufuta wenye ubora. Pia wana uhakika wa kuuza vizuri sokoni. Sasa ufuta wenu mnaandaa vizuri ndio sababu wanunuzi ingawa wapo mbali lakini wanashindania.


Hata hivyo mkulima Fatuma Chigope mkazi wa kijiji cha Nambilanje aliuliza kama ufuta wao ni bora kwanini unazidiwa bei na ufuta wa unaolimwa katika mikoa iliyopo katika kanda nyingine ikiwamo mkoa wa Songwe? 


Kadikilo alijibu kwakusisitiza kwamba ufuta wa mikoa ya Kanda ya Kusini ni bora bali kutofautiana bei kunasababishwa na mambo mengi. Ikiwa ni pamoja na kuanza misimu ya mavuno na mauzo.


" Sababu ni nyingi. Kufika mahali ulipo ufuta, uhitaji wa soko, gharama za usafirishaji na muda wa mauzo. Kwamfano huko Songwe wameanza kuuza mwezi Aprili," alisema Kadikilo.


Alisema mwezi Julai nchi nyingi zinauza ufuta. Kwahiyo kwenye soko la dunia kuna kuwa na ufuta mwingi. Hali ambayo inasababisha bei kupungua.


Amesema iwapo ufuta wa mikoa hii usingekuwa bora bei zingekuwa ndogo sana kuliko za sasa. Lakini pia ufuta wa mikoa hii ungekuwa unavunwa na kuuzwa mwezi Machi, Aprili na hata  Mei ungeweza kununuliwa hata kwa zaidi ya shilingi 5,000 kwa kilo moja kutokana na ubora wake.


Aidha Kadikilo aliweka wazi kwamba katika miezi ya Julai wanunuzi wengi wanaelekeza nguvu nchini Msumbuji. Ni kutokana na aina ya ufuta unaolimwa nchini humo ambao ni mweupe.

Post a Comment

0 Comments