Na Mwandishi Wetu
WAENDESHA pikipiki zaidi ya 160 katika Wilaya ya Handeni mkoani Tanga wamepatiwa mafunzo ya usalama barabarani kuondokana na changamoto za ajali za barabarani zinazotokana na kutozingatiwa kwa sheria.
Mafunzo hayo yanatolewa na Shirika la Amend kupitia ufadhili wa ubalozi wa Uswis nchini, lengo lake ni kupunguza ajali za barabarani kwa kundi la vijana wanaojihusisha na usafirishaji abiria kwa usafiri wa pikipiki (pikipiki).
Akizungumza apipotoa mafunzo kwa waendesha pikipiki, Kaimu Kamanda wa Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, Inspekta Gwantwa Mwakisole amesema ni muhimu kuoa maisha ya bodaboda kwa kukabiliana na ajali za barabarani.
“Mafunzo ya usalama barabarani yanayotolewa na wenzetu wa Amend kwa kushirikiana na ubalozi wa Uswis nchini ni muhimu sana kwa vijana wanaondesha pikipiki, hapa kwetu imepita barabara kuu inayounganisha mkoa wetu na mikoa mingine, hivyo ajali za bodaboda kugongwa zinatokea mara kwa mara.
“Kupitia mafunzo haya tunaamini tunakwenda kupunguza ajali lakini niowambe waendesha pikipiki kuzingatia sheria za usalama barabarani. Hata hivyo tunaomba mafunzo haya yaendelee kutolewa Handeni ili vijana wengi wapate uelewa wa sheria hizi,” amesisitiza.
Kwa upande wao waendesha pikipiki ambao wamepatiwa mafunzo hayo, wametumia nafasi hiyo kulishukuru Shirika la Amend na Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani kwa kuwapatia mafunzo hayo kwani yamewawezesha kufahamu sheria na alama mbalimbali za barabarani.
“Wengi wetu tunaendesha pikipiki kwa mazoea, hatuna elimu ya usalama barabarani, hivyo ajali zimekuwa nyingi. Kupitia mafunzo haya sasa tutakuwa makini barabarani lakini tutahakikisha tunakuwa mabalozi wazuri kwa wenzetu ambao hawajapata mafunzo haya,” amesema Jamali Mhando.
Wakati huo huo, Ramadhan Nyanza ambaye ni Mratibu wa Shirila la Amend Tanzania, amesema jumla ya maofisa usafirishaji (bodaboda) 160 wamepatiwa mafunzo ya usalama barabarani na huo ni mwendelezo wa kampeni ya kupunguza ajali za barabarani kwa vijana nchini.
0 Comments