Wakulima na wafanyabiashara wa mazao walalamika kuhusu stakabadhi ghalani..

Na John Walter-Manyara

Wakulima na wafanyabiashara wa Mazao Mkoani Manyara wamepinga uamuzi wa Serikali wa kununua Mazao Kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani wakidai kuwa mfumo huo hauna tija  kwao na unatishia ushindani wa soko huria katika mazao ya Dengu na Mbaazi.

Kauli hiyo ya Wakulima na wafanyabiashara wa mazao inakuja siku chache baada ya mkuu wa mkoa Manyara kusisitiza mfumo huo kwa wafanyabiashara na wakulima kuhusu ununuzi wa mazao kwa stakabadhi za ghala kwa lengo la kuongeza tija na kumuinua mkulima ambaye anaonekana kuwa chini kila siku licha ya kutumia gharama kubwa kwenye kilimo.

Baadhi ya wafanyabiashara wa mazao na wakulima akiwemo John Maganga na Elsau Ibrahim wamesema mfumo wa stakabadhi ghalani umekiuka haki na uhuru wa Mkulima wa kujipatia soko lenye ushindani kwani unawalazimisha wakulima kuuza Mazao yao kwa mnunuzi mmoja huku wakiiomba Serikali kutafuta namna nyingine ili kukuza ushindani wa soko kwa kutoa fursa ya ununuzi wa mazao yao katika soko huria.

Mkulima mwingine Liberia Gaudence amesema ''shida ni mfumo haukuanzia chini kipindi mkulima analima anakutana na changamoto nyingi hasa katika viuatilifu hakuna uratibu mzuri unaoonyesha  kwamba mkulima anapopata changamoto kwenye Mazao yake hakuna mfumo unaotusadia kwahiyo tunaiomba serika mifumo ya kumsadia Mkulima kama ipo ianzie chini pale ambapo Mkulima anaratibu shughulia zake za kilimo na siyo kipindi Mkulima anavuna''

Naye Ibrahim Juma mussa  Makamu Mwenyekiti wa kilimo Biashara (TCCIA) Mkoa wa Manyara amesema wao ni kiunganishi kati ya Wafanyabiashara, Wakulima na serikali hivyo wamepokea changamoto ya Wakulima kuhusu mfumo wa ununuzi wa mazao Kupitia stakabadhi ghalani ambao wakulima na wafanyabiashara wamedai hauna ushindani.

Kwa upande wake Katibu mtendaji wa TCCIA mkoa wa Manyara Zainabu Sadiki Rajab amewataka wakulima na wafanyabiashara kutumia jukwaa hilo kutoa maoni yao na changamoto zinazowakabili ili ifikishe katika ngazi husika.

Post a Comment

0 Comments