Na John Walter -Babati
Wakazi wa mkoa wa Manyara wameombwa kuendelea kudumisha amani na utulivu kuelekea zoezi la kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura pamoja na uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu wa 2024, kwani amani na utulivu ni nguzo muhimu zitakazosaidia kutoa fursa kwa wananchi wote kushiriki kikamilifu.
Hayo yamesemwa leo septemba 1, 2024 na mkuu wa mkoa wa Manyara Queen Sendiga wakati akizindua rasmi zoezi la kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura kupitia hamasa aliyoipa jina la ‘Manyara Daftari Day’ iliyofanyika kwa njia ya matembezi kwenye wilaya zote za mkoa huo.
Aidha mkuu wa mkoa Sendiga amewaasa vijana na wanawake kujitokeza kwa wingi kugombea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa ili kupata viongozi wengi vijana wanaoweza kuchapa kazi na kuendana na kasi ya mabadiliko.
Uzinduzi huo uliofanyika katika uwanja wa Tanzanite Kwaraa Stadium ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa wa mkoa wa Manyara ili kuwa sehemu ya hamasa kwa kuwa nao ni moja ya wadau wakuu wa zoezi hilo linalotarajiwa kuanza tarehe 4-9 mwaka huu.
Athuman Isimbula ni mwenyekiti wa chama cha wananchi CUF jimbo la Babati mjini na kwa upande wake amewaasa wananchi wasiwe na hofu kwani mwaka huu sio wa kuogopa bali ni wa kupiga kura kwa uhuru na hiari kuchagua chama unachokitaka kwani jambo la muhimu ni kuleta mabadiliko.
‘Ninachokiomba kwenu ni kufanya harakati za kujiandikisha kwa wingi sana, tusiogope, mwaka huu sio wa kuogopa na nenda kwenye chama unachokitaka kwasababu tunachokitaka ni mabadiliko’.
Kwa upande wake mwenyekiti wa chama cha ACT Wazalendo jimbo la Babati mjini Issa Athuman Ally amesema lengo kubwa ni kuhamasisha wananchi wakajiandikishe, hivyo ushirikiano ni muhimu sana ili kufikia malengo yaliyokususdiwa kwasababu kuwepo kwa vyama vingi sio kufarakana.
‘Tushirikiane katika hilo ili tuweze kufikia malengo kwasababu lengo la vyama vingi sio kugombana, sio kufarakana bali nikufikia yale malengo yaliyokusudiwa’.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA nao hawakuwa nyuma, walihudhuria kwenye hafla hiyo wakiwakilishwa na katibu msaidizi wa chama hicho jimbo la Babati mjini ambaye amesisitiza zaidi kutokuangalia itikadi za vyama bali wananchi wajiandikishe kwenye daftari lakudumu la wapiga kura ili kuchagua kiongozi wanaomtaka.
‘Nawasihi wananchi wote wa mkoa wa Manyara bila kuangalia itikadi ya chama chochote ambacho unatokea, twendeni tukajiandikishe na tukishajiandikisha tukachague kiongozi tunaemtaka sisi na sio wanaomtaka wao’.
Manyara Daftari imekwenda sambamba na kauli mbiu isemayo ‘Imarisha afya, jiandikishe na chagua viongozi wa serikali za mitaa kwa ujenzi wa jamii endelevu’ ikiwa ni sehemu ya kutoa hamasa kwa wananchi wa mkoa wa Manyara ili kushiriki kikamilifu kwenye zoezi hilo.
Ikumbukwe kuwa kwa mkoa wa Manyara wilaya za Simanjiro na Kiteto hazitoshiriki katika zoezi hilo kwa awamu hii bali zitashiriki kwa kuungana na mkoa wa Kilimanjaro kama ratiba ya tume huru ya uchaguzi inavyoelekeza.
Zoezi la kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura kwa awamu ya pili litajumuisha mikoa ya Manyara, Mara na Simiyu wakati zoezi la awali kabisa lililoanza tarehe 20 mwezi Julai mwaka 2024 lilijumuisha mikoa ya Kigoma, Tabora ,Katavi, Geita, Kagera, Mwanza na Shinyanga.
0 Comments