Samia na Gekul Cup 2024 kuibua vipaji vya soka mjini Babati.



Na John Walter -Babati 

Mbunge wa jimbo la Babati mjini Mheshimiwa Paulina Gekul, ametangaza ujio wa mashindano ya mpira wa miguu yatakayoanzia ngazi ya vijiji na mitaa kwenye jimbo la Babati mjini yaliyopewa jina la ‘Mama Samia na Gekul Cup’.

Akizungumzia mashindano hayo, Mhe. Gekul amesema lengo kubwa ni kuinua vipaji vya soka mjini Babati na kutumia fursa iliyopo ya uwanja wa Tanzanite Kwaraa pamoja na fountain gate FC waliopo mjini humo ambao wana shule kwa ajili ya kukuza vipaji hivyo.

Katika kufanikisha hilo, Mhe. Gekul amegawa jezi na mipira kwa gharama zake katika mitaa na vijiji vyote vya Jimbo la Babati mjini.

Aidha amesema ujio wa mashindano hayo ni sehemu ya kuiunga mkono serikali ya awamu ya sita inayothamini michezo chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan pamoja shirikisho la mpira wa miguu hapa nchini (TFF) kwa juhudi za kuendelea kukuza sekta ya michezo ikiwemo kuukubali uwanja wa Tanzanite Kwaraa kutumika kwenye mashindano ya ligi kuu Tanzania bara.

Gekul amesema baada ya kukamilisha ujenzi wa uwanja sasa ni zamu ya kuwapa fursa vijana kuonesha vipaji walivyonavyo ili wapate nafasi ya kusajiliwa na timu za ligi kuu hapa nchini na kupunguza changamoto ya uwepo wa vijana wengi wasiokuwa na ajira lakini pia kupata timu ya mkoa wa Manyara itakayoshiriki ligi kuu.

"Lengo letu pia na sisi tuwe na timu ambayo inacheza ligi kuu, na tutaifikia kwa kuibua vipaji huko chini ambapo vijana wetu wapo, hivyo sisi chama na serikali pamoja na viongozi wa timu tunakwenda kuanza mashindano haya katika jimbo zima" alisema Gekul 

Kwa upande wake mwenyekiti wa chama cha mpira wa miguu wilaya ya Babati (BDFA) Gerald Mtui amesema wameyapokea vizuri mashindano hayo kwani lengo kubwa ni kuhakikisha vipaji vipya vya Soka vinapatikana na watahakikisha wanalisimamia hilo ipasavyo.

Mratibu wa mashindano hayo katibu wa Mbunge Abrima Hussein amesema timu 48 kwenye mitaa na vijiji pamoja na 29 za taasisi mbalimbali zilizopo Babati mjini zitashiriki katika michuano hiyo mikubwa ya Mama Samia & Gekul Cup.

Mashindano ya Mama Samia na Gekul Cup yataanza kwa timu za mitaa na vijiji kwenye kila kata kuchuana na baadae kupata mshindi kwa kila kata na hatimaye kila kata kuchuana na kupata mshindi wa jumla wa jimbo la Babati mjini.

Post a Comment

0 Comments