Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) PROF. NAJAT KASSIM MOHAMMED amesema taasisi hiyo itakuwa mlezi wa programu maalumu ya diploma ya masomo ya teknolojia ya nyuklia itakayoanzishwa na chuo cha ufundi Arusha (ATC).
Prof. Najat ameyasema hayo katika ofisi za TAEC kanda ya kaskazini eneo la Njiro jijini Arusha baada ya kufanya kikao cha pamoja Kati ya uongozi wa TAEC na uongozi wa chuo cha ufundi Arusha kwa lengo la kuanza maandalizi ya kuanzisha diploma hiyo ya masomo ya nyuklia ambapo TAEC itakuwa mlezi kwa kutoa wataalamu wake watakaoongoza mchakato wa kuwezesha mtaala wa masomo hayo kufanikiwa.
Prof. Najat ameongeza kuwa TAEC kwa kuwa ina wataalamu wa teknolojia ya nyuklia imetenga muda wa mwaka mmoja kwa kushirikiana na chuo cha ufundi Arusha kwa ajili ya kuwaandaa walimu wa chuo hicho kwa kuwapatia mafunzo kwa njia ya nadharia na vitendo ili kuwajengea uwezo walimu watakaokuwa na dhamana ya kufundisha masomo hayo.
Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania ndiyo taasisi pekee ya serikali iliyopewa dhamana ya kusimamia matumizi salama ya mionzi nchini, kuhamasisha na kuendeleza teknolojia ya nyuklia katika sekta mbalimbali kama vile afya, kilimo, mifugo, nishati, migodi, viwanda, maji na kufanya tafiti mbalimbali kwa kutumia Teknolojia ya Nyuklia sambamba na kutoa ushauri kwa serikali juu ya mikataba mbalimbali ya kimataifa inayohusisha matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia.
0 Comments