Airtel Tanzania imeingia ushirikiano wa miaka miwili na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ili kusaidia katika mchakato wa kuvutia wawekezaji wa ndani na Wakimataifa.
Ushirikiano huu kati ya TIC na Airtel Tanzania unaonyesha dhamira ya taasisi hizi katika kuwezesha ukuaji wa kiuchumi wa Tanzania kwa kuweka mazingira bora `ya uwekezaji.
Akizungumzia ushirikiano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC, Gilead Teri alisema kuwa ushiriki wa Airtel Tanzania utaonyesha jinsi Kituo cha Uwekezaji Tanzania kitakavyotumia huduma za mawasiliano na TEHAMA kwa ufanisi kushughulikia maswala mbalimbali yanayolenga kuboresha uwekezaji nchini Tanzania.
"Airtel Tanzania inamilikiwa na serikali kwa asilimia 49, hivyo ushirika huu unadhihirisha dhamira ya Airtel katika kuhudumia taasisi za serikali na kuchagiza ukuaji wa uchumi wa Tanzania kupitia uwekezaji. Katika kipindi cha miaka miwili ijayo, kupitia ubia huu kati ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC na Airtel Tanzania utasaidia kuboresha matokeo chanya kwa taifa letu,'' Teri aliongeza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Dinesh Balsingh, alisisitiza kwamba ushirikiano huo utasaidia ukuaji wa uchumi wa Tanzania na kuwezesha maendeleo ya nchi katika uchumi wa kidijitali, kukuza mwingiliano mzuri na kuvutia wawekezaji wapya.
“Ushirikiano huu unakuja wakati muafaka baada ya Airtel kuwa tumeanzisha Mkongo wa chini ya bahari wa Airtel 2Africa kwa lengo la kuleta mapinduzi katika sekta ya teknolojia. Mkongo huu wa chini ya bahari wa Airtel 2 Africa utaifanya Tanzania kuwa kitovu cha kidijitali, na hivyo kuimarisha ushirikiano kati ya TIC na wawekezaji wapya duniani,’’ Balsingh alifafanua.
Balsingh alieleza zaidi kuwa kutokana na mawasiliano imara ya Airtel, TIC itakuwa katika nafasi nzuri ya kuvutia wawekezaji kwenye soko la Tanzania na kuongeza idadi ya miradi ya maendeleo iliyoandikishwa na kituo hicho cha uwekezaji.
Pia aliongeza kuwa ushirikiano wa TIC na Airtel unawawezesha wawekezaji wazawa kufanya malipo kwa urahisi ili kulipia gharama mbalimbali zinazohusiana na TIC kama vile usajili kupitia huduma ya Airtel Money.
0 Comments