Na John Walter- Hanang'
Serikali kupitia wizara ya Maji Nchini imeombwa kutoa shilingi bilioni 1.5 iliyobaki ili kukamilisha Mradi wa maji kwa wakazi wa Katesh waliokumbwa na adha ya maporomoko ya tope,mawe na magogo kutoka mlima Hanang' mwishoni mwa mwaka jana.
Ombi hilo limetolewa na mkuu wa wilaya ya Hanang' Almish Hazali alipotembelea miradi ya maji inayotekelezwa na BAWASA katika wilaya hiyo.
Aidha Almish amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuirudisha Hanang' kwenye hali yake ya kawaida mara baada ya kukumbwa na Maporomoko makubwa.
Mkuu wa wilaya pamoja na kamati yake ya ulinzi na usalama wameridhishwa na mwenendo wa mradi huo wa maji unatekelezwa na BAWASA akiisisitiza wizara ya Maji kuharakisha upatikanaji wa fedha kiasi cha shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya umaliziaji.
Mamlaka ya maji safi na usafiri wa Mazingira Mjini Babati (BAWASA) ambayo inahudumia wilaya ya Hanang' , imesema shilingi Bilioni 1.5 ikipatikana mji wa Katesh unaoundwa na kata nne za Katesh, Jorodom Dumbeta na Ganana, utapata maji kwa asilimia 100 kabla ya Juni mwaka 2025.
Licha ya maporomoko ya tope la Desemba 3, 2023 kuacha simanzi kwa wakazi wa Hanang' kwa kupoteza ndugu na jamaa zao na kuwaacha mamia bila makazi, miundombinu mbalimbali ikiwemo ya maji haikusalia salama, hivyo kupelekea serikali kujenga miradi ya maji ukiwemo wa Jorodom, Dumbeta ambao chanzo chake ni eneo la hifadhi ya mlima Hanang' ambao utekelezaji wake ulianza Mwezi Juni 30, mwaka 2024.
Mkurugenzi wa mamlaka ya Maji safi na usafi mazingira mjini Babati Mhandisi Iddi Msuya ameeleza kuwa mradi huo unagharamiwa na Serikali ya awamu ya sita kwa shilingi bilioni 4.452 na utakapokamilika utawahudumia zaidi ya wananchi elfu thelathini na tano.
"Tulianza na kazi ya kujenga chanzo ambapo kwa sasa kimekamilika kwa asilimia 97,halafu tuakafanya kazi ya kulaza hili bomba kuu la nchi 12 kwa urefu wa kimomita 1.5" alisema Mahandisi Msuya
Mhandisi Msuya amesema mpaka sasa Mradi unatoa huduma ya maji kwa zaidi asilimia 92 kwa wakazi wa Katesh na jitihada zinazoendelea ni kupeleka huduma kata za Jorodom na Dumbeta.
Vijana 19 wanaofanya kazi kama vibarua kwenye mradi huo, wamemshukuru Rais Dkt Samia kwa kuendelea kutoa pesa za miradi kwa kuwa inawasaidia nao kupata fedha zinazowasaidia wao na familia zao.
Wilaya ya Hanang' ilikumbwa na maporomoko ya tope mawe na magogo kutoka mlima Hanang' na kuathiri miundombinu ya Maji na mingine.
0 Comments