F Kwanini Wananchi wengi hawatoi ushahidi kwenye kesi za ukatili? Fuatilia makala hii kujua sababu hizo na suluhisho lake.. | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Kwanini Wananchi wengi hawatoi ushahidi kwenye kesi za ukatili? Fuatilia makala hii kujua sababu hizo na suluhisho lake..


Na Samson Mgelwa -Manyara 

Matukio ya kikatili yameendelea kukithiri kwa wingi sana nchini Tanzania na Duniani kwa ujumla na hii ni kutokana na ripoti mbalimbali za vyombo vya habari na taasisi za serikali na zisizo za kiserikali kufanya kampeni mbalimbali ili kuhakikisha ukatili unatokomea kwa kuwabaini waliofanya ukataili huo nakuwafikisha kwenye vyombo vya sheria ili sheria ifuate mkondo wake.

Lakini imeonekana katika mwenendo wa kesi hizo washtakiwa huachiwa huru kwa kukosekana kwa ushahidi wa kutosha wa kumtia hatiaani mtuhumiwa na mwishowe anarudi uraiani na kuendelea na maisha mengine, sasa katika Makala hii tutaangazia kwanini wananchi wengi hawatoi ushirikiano kwa jeshi la polisi pale mtuhumiwa wa kosa la ukatili anapokamatwa?

Kwa mujibu wa takwimu za umoja wa mataifa zimeonesha ukatili dhidi ya wanawake umeongezeka kwa miaka ya hivi karibuni hasa ukatili wa kingono kwani inakadiriwa takribani wanawake milioni 736 wamepitia changamoto ya ukatili wa kingono kutoka kwa wapenzi wao na wasio wapenzi wao au vyote kwa ujumla, na asilimia 30 ni wasichana wenye umri wa miaka 15 pamoja na vikongwe na kwa wastani kati ya wananwake 3 mmoja amefanyiwa vitendo vya ukatili wa kingono.

Lakini pia mwaka 2022 takwimu za umoja wa mataifa zimeonesha karibia wanawake 48,800 wameuawa na wapenzi wao au watu wa karibu wa familia hii ikimaanisha kwa wastani zaidi ya wanawake na wasichana watano wanauawa kila baada ya saa moja na watu waliopo kwenye familia zao.

Nchini Tanzania kwa mujibu wa ripoti ya mfuko wa kimataifa wa watoto wa umoja wa mataifa UNICEF ya mwaka 2023 imeonesha msichana 1 kati ya 3 na mvulana 1 kati ya 7 wameathiriwa na ukatili wa kingono na vilevile zaidi ya vijana wadogo 7 kati ya 10 wamekumbana na ukatili wa kimwili kutoka kwa familia au jamii zao wanamoishi.

Ripoti hizi hazirkuishia hapo tu bali pia zimeeleza athari wanazopitia wanawake, wasichana na watoto baada ya kukumbwa na changamoto hizo za vitendo vya kikatili ikiwemo kupata msongo wa mawazo, mimba zisizotarajiwa, maambukizi ya magonjwa na virusi vya UKIMWI na matatizo ya wasiwasi yanayopelekea kupata athari za muda mrefu.

Mkoa wa Manyara ni mkoa wa pili kwa ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto nchini Tanzania, kwa mwaka 2022 mkoa wa Manyara ulikuwa na matukio ya ukatili 5912, mwaka 2023 kulikuwa na matukio ya ukatili 8360 na kwa mwaka huu wa 2024 tangu mwezi januari hadi kufikia mwezi Agasti kulikuwa na matukio 6261 na takwimu hizi ni kwa mujibu wa mfumo wa afya wa kutolea taarifa.

Utitiri wa matukio haya ya ukatili unaonesha wazi ni kwa kiasi gani matukio haya yamekithiri nchini Tanzania na ulimwenguni kote kwa ujumla, lakini kuna changamoto ya watu kutokutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi pindi kesi za ukatili zinapofikishwa kwenye vyombo vya sheria na hili linathibitishwa na Ramadhan Mangi mwenyekiti wa kijiji cha Matufa kilichopo kata ya Magugu wilaya ya Babati mkoa wa Manyara.

"Nimeshasimamia kesi tano za ukatili na ninaishukuru mahakama ya wilaya kwasababu kule nimeshakwenda hadi mara nne, nimewapeleka watu kule na kesi mbili zilipitiwa na hukumu ilitoka na washtakiwa walifungwa lakini kesi zingine mbili mashahidi walikataa kutoa ushahidi kabisa na hilo ndio tatizo kubwa sana ambalo mimi nalililia katika jamii ninayoingoza sasa hivi ndani ya kijiji changu, ushahidi umekuwa ni chanzo cha matatizo makubwa sana, watu wanakwepa kutoa ushahidi"

Baada ya mwenyekiti wa kijiji cha Matufa kuelezea changamoto hiyo ya wananchi kukwepa kutoa ushahidi mahakamani ikanilazimu kufunga safari hadi kata ya Bashnet iliyopo tarafa ya Bashnet eneo ambalo pia matukio mengi ya kikatili yameripotiwa ikiwemo mauaji na ubakaji wa vikongwe, wasichana na watoto ili kujua kwanini wanakwepa kutoa ushahidi mahakamani.

Petro Amsi ni mwananchi wa kata ya Bashnet kwa upande wake amesema changamoto ipo kwa jeshi la polisi kwani pale mwananchi anapotoa ushahidi anakamatwa na kupelekwa kituo cha polisi hali inayozua hofu kwa wananchi na kupendekeza kama mwananchi atatoa ushahidi basi asikamatwe.

"Lakini sasa kwa polisi inakuwa ni hatua ya kwanza ya kumkamata huyohuyo na swali la kwanza ni kwamba umemjuaje huyo mtu, badala ya kukuhoji hapa na kukuacha hapahapa ukarudi kwa watu wako, wanakupeleka kituoni na kukuhoji huko ili kupata wengine, sasa ndo maana hata mtu akiuawa pale kikatili hata kama kuna mmoja alikuwa anawaona kule hatosema maana atasumbuliwa sana.” Petro Amsi mwananchi.

Kwa upande wake Agatha Samweli mwenyeji wa kata hiyo ya Bashnet amesema wanaogopa kutoa ushirikiano kwa kuhofia aliyetenda kosa hilo akitoka atawarudia na wao kwasababu kesi nyingi watuhumiwa wanaachiwa huru na kama kesi za ukatili kifungo chake ni miaka 30 basi mahakama zitekeleze hukumu hiyo.

"Sasa nikwambie, kuna mtoto mmoja alifanyiwaga ukatili hapa Bashnet alibakwa na alitolewa kizazi kule hospitali na mtuhumiwa aliyefanya hilo jambo alifkishwa hapa polisi na kupelekwa Babati, lakini mtu aliyefanya ubakaji siwanasema kifungo chake ni miaka 30? Lakini yeye aliachiwa kwa dhamana na wazazi wake wakamtorosha wakampeleka Handeni na ndio maana sisi huku tunaogopa kutoa ushahidi kwani akitoka atakurudia na wewe.” Agatha Samweli mwananchi"

Josephina Samweli ni mama wa watoto wa tatu mkazi wa kijiji cha Diffir ambae amepitia changamoto kadhaa za ukatili kwenye familia yake ikiwemo kupigwa na mume wake na kushuhudia watoto wake wakipewa adhabu kali na mume wake lakini ameshindwa kutetea kwa kuhofia ndoa yake kuvunjika na pia kupokea vitisho kutoka kwa jamii yake endapo atatoa ushahidi wa kesi yeyote ile ya ukatili.

"Sasa tunaogopa ukirudi huko kutoa ushahidi utauawa bure tu, kwasababu huyo mtu akienda huko anakaa miezi miwili, mitatu anarudi na mzee anapiga mtoto we ukienda kumsaidia anakutishia mara nitakuua mara ntakupa sumu, na mimi nitaendaje kusema, ukishaenda kusema mahakamani ni moja kwa moja unaondoka sasa familia yako unaiacha bure na utaenda kuishi wapi?"

Kuna sheria mbalimbali za kulinda na kupinga ukatili nchini Tanzania ikiwemo sheria ya kuzuia ukatili wa kijinsia ya mwaka 2008, sheria ya watoto ya mwaka 2009, na sheria ya kuzuia na kudhibiti unyanyasaji wa wanawake ya mwaka 2016.

Kifungu cha 3 cha sheria ya kuzuia ukatili ya mwaka 2008 kinabainisha aina za ukatili wa kijinsia kama vile unyanyasaji wa kimwili, kingono na kiakili, lakini pia kifungu cha 6 kinatoa adhabu kwa wahalifu wanaofanya vitendo vya ukatili wa kijinsia na adhabu zake zinaweza kuwa jela miaka 30 au zaidi kulingana na ukali wa tendo lenyewe.

Ukiachilia mbali sheria hizi za masuala ya ukatili lakini pia zipo sheria zinazowalinda mashahidi kwenye kesi za ukatili ikiwemo sheria ya usalama wa mashahidi ya mwaka 2013 ikiwa ni pamoja na kuhamasisha ulinzi wa kimwili na faragha kwa mashahidi wa kesi nyeti.

Kutokana na sababu hizi kuntu kutoka kwa wananchi wakieleza kwanini hawatoi ushahidi kwenye kesi za ukatili ikanilazimukamanda wa polisi wilaya ya Babati OCD Ernesta Mwambinga ili kujua ni namna gani wanaweza kusimamia sheria ya kuwalinda mashahidi ili waweze kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi kwenye kesi mbalimbali za ukatili ili iwe rahisi kuwatia hatiani watuhumiwa wa kesi hizo na kuondoa kabisa idadi ya vitendo vya ukatili kwenye jamii, na kueleza kuwa wananchi waondoe hofu juu ya usalama wao na kama anahisi kuna changamoto kwenye jamii yake atoe taarifa ili wajue namna ya kumsaidia kwani sheria inamlinda hivyo wasifiche vitendo vya ukatili.

"Wale watu wanavyochukuliwa hatua inatusaidia sisi na wananchi kwa ujumla kujua kama vitendo vipo au havipo na wale wote watakaoonekana wamekutwa na hatia dhidi ya vitendo vya ukatili wataenda jela namashahidi wa kesi hizo watalindwa maana zipo sheria za kuwalinda mashahidi na kama kuna changomoto yeyote  wananchi watoe taarifa ili tujue namna ya kuwasaidia"

Kutokana na changamoto hiyo mwanasaikolojia Robert Lwiza ameeleza kuwa ukatili kwa kiasi kikubwa unawaathiri sana wanawake na unafanywa kwa kiasi kikubwa na wanaume ambao wanaonekana wana nguvu kwenye jamii na hiyo ndiyo sababu inayofanya wanaogopa kutoa ushahidi kwenye kesi kwasababu wenye nguvu kwenye jamii ndio chanzo cha ukatili na wanamamlaka kwenye familia.

"Mwanaume mmoja anaweza hata akawadhalilisha wanawake 10 au 15 na wanawake wengi wanapitia changamoto kutokana na kwamba wanaofanya hivyo ni baadhi ya watu ambao hawana hisia na wanawake na pia mila na desturi zinachangia kwahiyo waathirika wengi ni wananwake na inakuwa ngumu kutoa ushahidi kwenye kesi za aina hiyo."



Kwa kiasi kikubwa ukatili unafanywa na watu wa kwenye familia kama takwimu zilivyeleza na kutokana na sababu hizo ukatili unahusishwa sana na suala la malezi kwenye familia kama alivyobainisha Naibu waziri wa mambo ya ndani ya nchi Daniel Sillo akiwa kwenye mahafali ya kidato cha nne shule ya sekondari Matufa kuwa ili kutokomeza ukatili wazazi watimize wajibu wao wa malezi kwa kuwalea vijana kwenye misingi mizuri na kuacha kasumba za usasa zinazoleta athari kubwa.

“Naomba wazazi wenzangu tusikimbie wajibu huu, tuwalee watoto kwa njia ipasavyo, leo hii matukio yanatokea tunalaumu wazazi kuwa watoto wa siku hizi je hao watoto wa siku hizi wametoka wapi? Bila shaka na wao wametokana na wazazi wa siku hizi, kwahiyo turudi kwenye majukumu ya msingi, tuzungumze kwa uwazi na tuwaleeze hali ya dunia inavyokwenda, unaposikia kijana mdogo anabaka bibi kizee sisi tuko wapi na tunajitengaje na hiyo dhambi? Kwahiyo naomba wazazi tuzungumze na watoto wetu.”

Hadi kufikia hapa bila shaka changamoto ya wananchi kukwepa kutoa ushahidi itapungua kwani usalama wa shahidi unalindwa kwa mujibu wa sheria kama zilivyelekeza na wananchi waondoe hofu lakini pia kuongeza jitihada za malezi bora kama vyanzo vyetu vilivyoeleza ili kupunguza vitendo vya ukatili, hivyo basi ni vyema kila mmoja asimame kwenye nafasi yake huku tukimtanguliza MUNGU katika kila jambo na mioyo yetu ibebe utu pamoja na hofu yaki MUNGU ili kunusuru kizazi kijacho.

Na kufikia hapo ndio mwisho wa Makala hii iliyoangazia kwanini wananchi hawataki kutoa ushahidi kwenye kesi mbalimbali za ukatili, bila shaka umejifunza mengi jina langu ni Samson Mgelwa hadi wakati mwingine.


Post a Comment

0 Comments