Na John Walter -Babati
Baada ya jitihada mbalimbali kufanyika bila mafanikio huku wazazi wakikata Tamaa, hatimaye Mtoto Joel Mariki (15) mwanafunzi wa kidato cha pili shule ya Sekondari Bagara mjini Babati mkoa wa Manyara amepatikana akiwa hai.
Joel amepotea tangu septemba 14 na kuonekana siku ya Oktoba 9 ambayo inakuwa siku ya 26 tangu apotee katika mlima Kwaraa alipoenda na Wanafunzi wenzake pamoja na walimu kwa ajili ya kujifunza kwa vitendo.
Taarifa za kupotea kwake ziliripotiwa kituo cha polisi Babati ambapo jitihada za kumtafuta zilifanyika kwa kushirikiana na jeshi la zimamoto na uokoaji bila mafanikio.
Oktoba 9 majira ya asubuhi wazazi walipokea simu kuwa mtoto anaefanana na Joel ameonekana Kijiji cha Galapo ambapo baada ya kufika walimkuta tayari amefikishwa hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Manyara na kubaini ni kweli ni mtoto wao waliyekuwa wanamtafuta.
Walimkuta na michubuko ,majeraha miguuni huku mwili ukiwa umedhoofu Sana hali iliyoonesha kuwa alikuwa porini kwa siku zote hizo .
Kwa sasa Joel anaendelea na matibabu hospitalini hapo ili aweze kurejea katika hali yake ya kawaida.
Familia ya Joel imetoa shukrani kwa wote waliosaidia kupaza sauti za kumtafuta mtoto wao.
Mkuu wa wilaya ya Babati Emmanuela Kaganda amesema mtoto huyo amepatikana na raia Mwema ambaye alimfikisha hadi hospitalini.
0 Comments