F Nyaraka za usimamizi wa maafa zazinduliwa wilayani Hanang' | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Nyaraka za usimamizi wa maafa zazinduliwa wilayani Hanang'


Na John Walter -Manyara 

Kamati ya Wataalamu iliyoundwa kuchunguza chanzo cha kutokea maporomoko ya udongo,mawe na tope katika mlima Hanang' imebaini kuwa chanzo kilikuwa mipasuko ya miamba iliyohifadhi maji ya mvua iliyonyesha mfululizo kushindwa kuhimili na kusababisha udongo kuanza kuserereka na kuleta maafa kwa wananchi . 

Hayo yamebainishwa Oktoba 7,2024 na Mkurugenzi wa huduma za Jiolojia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania( GST) Dkt  Ronald Massawe wakati akitoa ufafanuzi wa matokeo ya utafiti wa kamati ya wataalamu iliyoundwa na kitengo cha maafa ofisi ya Waziri Mkuu na kuwasilishwa kwa wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang. 

"Kwenye ule mlima kule juu kuna structures kubwa na nyingine  ndogo sasa izo ndogo ndogo mvua zinapenyesha maji yanaenda kujihifadhi mle, kwa hiyo kuna lea ndogo sana ya udongo lakini miamba nayo imechanika ikahifadhi hayo maji kuanzia kwenye structures ndogo na kubwa (miamba iliovunjika ) Matokeo yake sasa unafika mahali ule mlima unashindwa kuhimili, ikitokea distabansi hata kidogo unaserereka kwa sababu maji yanalainisha miamba" alisema Dkt Massawe

Amesema mlima Hanang' ni miongoni mwa milima iliyopo katika mkatiko au ufa wa Balanginda wa ukanda wa kaskazini wa bonde wenye miamba yenye mipasuko mingi inayohifadhi maji ambayo siku chache kabla ya kutokea maporomoko ya Disemba 3, 2023 ilijaa maji kutokana na mvua zilizonyesha mfululizo iliyosababisha  kumeguka na kuanza kuserereka na kusababisha maafa. 


Mkuu wa Wilaya ya Hanang' Almish  Hazali ametoa pongezi na kushukuru  kwa taarifa hiyo ambayo amesema imeleta mwanga unaoweza kusaidia kuelimisha wananchi na kwamba Serikali inaendelea kuangalia tatizo hilo na kushughulikia kwa haraka.

"Kwa hiyo tunatakiwa kuwa makini mda wote,yaani tujihadhari na tuko tayari kutoa Elimu kwa wananchi na pia tutajitajidi kuotesha miti maana maeneo ambayo hayana miti yameleta athari Katika maeneo hayo". Alisema Almishi 


Uwasilishaji wa ripoti hiyo ya utafiti wa chanzo cha maporomoko ya udongo na mawe kutoka mlima Hanang'  imeenda sambamba na uzinduzi wa nyaraka ya usimamizi wa maafa, ambapo Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Maafa Dkt Jim Yonaz aliyekuwa Mgeni rasmi ameelekeza wataalamu wa Halmashauri ya Hanang kuzingatia ili kusaidia kupunguza athari ya maafa kwa siku sijazo. 

"Leo tumefanya tathimini ya maafa yaliyotokea na hiyo yote imetusaidia Serikali kupata uelewa, tunamshukuru kupata ripoti ya tathimi hiyo,tumezindua nyaraka mbalimbali za kutuongoza
Namna ambavyo kamati itakavyokabiliana na maafa kwa wilaya ya Hanang'  namna itafanya kazi" alisema Dkt Yonazi

Inaelezwa kuwa ripoti ya kina ambayo tayari imezinduliwa  ilifanyika April 2024 na kukamilika Mei 2024.

Post a Comment

0 Comments