F Serikali yajipanga kukabiliana na Maafa. | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Serikali yajipanga kukabiliana na Maafa.



 Na John Walter - Hanang' 

Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dkt. Jim Yonazi leo Oktoba 7, 2024 amekabidhi nyaraka za usimamizi wa maafa za Halmashauri ya Wilaya ya Hanang pamoja na taarifa ya tathmini ya Jiolojia, Haidrolojia na Mazingira.

Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang'  na kuhudhuriwa na Wajumbe wa Kamati Elekezi ya Usimamizi wa Maafa ya mkoa na wilaya, Wajumbe wa Kamati ya Watalaamu ya Usimamizi wa Maafa ya Mkoa wa Manyara na Wilaya ya Hanang, Wakuu wa Idara na Taasisi mbalimbali, Wataalamu kutoka Wizara, wakuu wa Idara na Taasisi za Serikali wilayani humo. 

Awali Dkt. Yonazi amesema miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuwekwa kwa mfumo wa kisera, kisheria na kitaasisi wa utaratibu wa masuala ya maafa kwa kutunga Sera ya Taifa ya Menejimenti ya Maafa ya mwaka 2004 na Sheria ya Usimamizi wa Maafa, Na. 6 ya mwaka 2022 lengo likiwa  ni kuendelea kuimarisha masuala ya usimamizi wa maafa.

Amefafanua kuwa, Sheria hiyo imebainisha majukumu na imeweka mfumo wa usimamizi wa maafa kupitia Kamati za Usimamizi wa Maafa kutoka ngazi ya Taifa hadi Kijiji/Mtaa. 

"Natambua, kwa sasa Halmashauri inaendelea kutekeleza shughuli za kurejesha hali baada ya maafa makubwa yaliyosababishwa na janga la maporomoko ya ardhi katika mlima Hanang’, tarehe 03 Disemba, 2023, hvyo, nitumie fursa hii kuwapongeza kwa jitihada mnazoendelea nazo katika urejeshaji hali" Amesema Dkt Yonazi 

Aidha amesisitiza kuendelee kuchukuliwa jitihada mbalimbali ikiwemo kutoa elimu kwa jamii kuhusu namna ya kuzuia na kupunguza madhara ya majanga na kujiandaa na kukabiliana na maafa na kuwahamasisha wananchi kutokutekeleza shughuli za kiuchumi na ujenzi katika maeneo hatarishi kwa kuzingatia ushauri wa kitaalamu. 

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Hanang’ na Mwenyekiti wa Kamati Elekezi ya Usimamizi wa Maafa ya Wilaya Almishi Hazali, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara ameishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kwa namna ilivyolishughulikia janga la maporomoko ya tope yaliyotokea wilayani humo na kueleza kuwa hatua ya uzinduzi wa nyaraka hizo muhimu ni nyenzo muhimu katika kuendeleza jitihada za namna ya kukabiliana na majanga na maafa nchini.

Baada ya hafla hiyo, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dkt. Jim Yonazi ametembelea nyumba 109 Wareti zinazojengwa na Serikali kwa ajili ya waathirika wa mafuriko ya tope yaliyotokea Katesh Desemba 3, 2023.


Post a Comment

0 Comments