Na John Walter -Babati
Shilingi Bilioni 4.1 zimetolewa na Serikali kujenga shule ya Wavulana mkoa wa Manyara baada ya shule ya Wasichana Manyara kukamilika kwa shilingi bilioni 3.
Mkuu wa Wilaya ya Babati Mhe. Emmanuela Mtatifikolo Kaganda Oktoba 30, 2024 amezindua ujenzi wa Shule hiyo ambayo ni ya Bweni inayojengwa katika kata ya Mwada, Kijiji cha Ngoley Halmashauri ya wilaya ya Babati, kwa kushiriki kuchimba msingi wa madarasa ya Shule hiyo.
Ujenzi wa Shule hiyo ya Bweni ya Wavulana kwa Mkoa wa Manyara wilaya ya Babati ni Miongoni mwa Shule saba za Kanda zinazojengwa nchini kwa kipindi cha 2024/2025 kupitia mradi wa SEQUIP fedha zilizopokelewa katika shule mama ya Sekondari Mbugwe.
Mhe. Kaganda ameeleza kuwa ndani ya wilaya ya babati, hiyo ni shule ya pili mpya kupokea fedha nyingi ikiwa ni pamoja na Shule ya Wasichana iliyojengwa katika halmashauri ya Mji wa Babati na kufanya jumla ya shule zote mbili kupokea Bilioni Nane za ujenzi wa Shule hizo.
Kaganda amewataka wananchi na Viongozi kushikamana ili kufanikisha malengo ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, kukamilisha mradi huo haraka ili ifikapo Januari 2026 Wanafunzi waanze kuingia madarasani.
"Shule hizi zinajengwa nchi nzima ni bilioni za fedha ambazo Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amezitoa kwa ajili ya kuboresha na kufanya mageuzi makubwa kwenye sekta ya Elimu ndani ya nchi yetu, Sisi Mkoa wa Manyara na Wilaya ya Babati tumepewa Heshima kubwa Sana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Mkoa huu ameleta fedha za kujenga Shule mbili ya Wasichana, Shule ya Sayansi na Shule hii ya Wavulana ni upendo mkubwa sanaa" Mhe. Kaganda
Kwa upande wao wananchi wa Kata ya Mwada wamefurahishwa na ujenzi wa Madarasa hayo pamoja na Mabweni na kukiri kuwa usumbufu utaisha na watoto wao watasoma katika maeneo mazuri na kuongeza kasi ya maendeleo ya kijiji.
Vijana wanaopata Mafunzo ya jeshi la akiba (mgambo) katika kata ya Mwada, wamejitolea nguvu kazi katika kuchimba msingi kwa ajili ya kuanza ujenzi.
0 Comments