F Waziri Nchemba awakaribisha wawekezaji kutoka Italia | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Waziri Nchemba awakaribisha wawekezaji kutoka Italia



Na mwandishi wetu 

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ametoa wito kwa wawekezaji kutoka nchini Italia kutumia mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyopo hapa nchini kuwekeza mitaji yao katika miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii ili kukuza uchumi wa pande hizo mbili.

Dkt. Nchemba ametoa wito huo alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Italia hapa nchini Mhe. Giussepe Sean Coppola, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, Jijini Dar es Salaam.

Alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeweka vivutio mbalimbali vya uwekezaji na kuialika sekta binafsi ya Italia, kushirikiana na Serikali kwa kuwekeza katika ujenzi na uendeshaji wa miradi mbalimbali hapa nchini ukiwemo mradi wa Reli ya Kisasa wa SGR.

Kwa upande wake, Balozi wa Italia hapa nchini Mhe. Giussepe Sean Coppola, alimwagia sifa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kusimamia vizuri uchumi na maendeleo ya nchi ikiwemo kuunda tume ya kushughulikia changamoto za kikodi nchini.

Alisema kuwa anaamini matokeo ya Tume hiyo yataongeza chachu ya kufanyabiashara na uwekezaji hapa nchini hatua itakayochochea ajira, ukuaji wa uchumi na kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika kuchochea maendeleo ya nchi.

Aliahidi kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika Nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii kwa kuchangia utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo sekta ya kilimo kwa kuendeleza mnyororo wa thamani wa zao la kahawa chini.

Italia imekuwa mdau mkubwa wa maendeleo wa Tanzania kwa kufadhili miradi mbalimbali kupitia bajeti kuu ya Serikali, ikiwemo miradi ya maji, afya, mafunzo ya ufundi stadi na huduma katika sekta za utalii na hoteli, uchumi wa buluu na usawa wa kijinsia.

Post a Comment

0 Comments