F Zoezi la kujiandikisha kwenye daftari la Mkaazi Manyara linaeendelea vizuri. | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Zoezi la kujiandikisha kwenye daftari la Mkaazi Manyara linaeendelea vizuri.



Na John Walter -Babati 

Mkuu wa mkoa wa Manyara Queen Sendiga leo amejiandikisha katika daftari la Mkaazi katika mtaa wake anakoishi wa Mrara mjini Babati.

Zoezi la kujiandikisha kwenye daftari la Mkaazi ni maandalizi ya kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa baadaye Novemba 27, 2024 ambapo Watanzania watapata nafasi ya kuchaguliwa na kuchagua Viongozi wa vijiji, mitaa na vitongoji.

Sendiga amesema zoezi hilo haliwezi kukwamisha shughuli za kimaendeleo za watanzania kwani linachukua muda mfupi sana kukamilika na mwananchi hatokaa muda mrefu kwenye kituo, hivyo waondoe hofu ya upotevu wa muda.


Aidha amebainisha kuwa zoezi hilo halimuhitaji mwananchi kuwa na kitambulisho chochote bali ni yeye pekee na ataullizwa maswali machache na kisha ataendelea na shughuli zake za kilasiku.

"Utaratibu wa kujiandikisha ni mwepesi sana, jina lako mwaka wa kuzaliwa sahihi yako kisha unaenda nyumbani, unasubiri tarehe 27 kuja kupiga kura, hivyo wananchi wote wa mkoa wa Manyara tunawahamasisha mtoke huko mliko muende mkajiandikishe kwasababu chaguzi za serikali za mitaa ni muhimu sana kwa taifa kwasababu ndio mwanzo wa uundaji wa serikali."

Kwa upande wake mwandishi msaidizi wa kituo cha mtaa wa mrara Petzuma Mhina ameeleza kuwa hari ya wananchi kujitokeza ni kubwa na wananchi wamepata elimu ya kutosha na amewaomba wananchi waendelee kujitokeza katika siku zote 10 za kujiandikisha.

"Sifa zinazohitajika ili kujiandikisha ni kuwa raia awe mtanzania mwenye umri kuanzia miaka 18 na kuendelea, hivyo nawakaribisha wananchi wote hasa wa mtaa wa Mrara kujiandikisha kwenye daftari la makazi."

Adam Juma ni mwananchi wa mtaa wa Mrara uliopo wilayani Babati na anaeleza kuwa amefurahi sana kujiandikisha kwenye daftari la makazi kwasababu itampa nafasi ya kumchagua mwenyekiti wa mtaa wa Mrara na ni nafasi muhimu sana kwa mwananchi yeyote anayejitambua.

Uandikishaji wa daftari la makazi unaanza hii leo tarehe 11 hadi tarehe 20 mwezi wa 10 mwaka huu.

Post a Comment

0 Comments