F Airtel Tanzania wamtangaza Charles Kamoto kuwa Mkurugenzi mpya | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Airtel Tanzania wamtangaza Charles Kamoto kuwa Mkurugenzi mpya

Airtel Tanzania imemtangaza Charles Kamoto kuwa Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Airtel Tanzania kufuatia mabadiliko makubwa ya uongozi yaliyofanyika Airtel Africa kwa lengo la kukuza ufanisi wa operesheni za Airtel katika soko la Tanzania na nchi zingine barani Afrika.

Katika taarifa iliyotolewa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Airtel Africa Group, Sunil Taldar, alisema kuwa mabadiliko hayo ya uongozi ni mkakati unaoendana na matarajio ya Airtel Group katika kuongeza nafasi ya Airtel katika soko la Tanzania na kuchagiza maendeleo endelevu kama mtoa huduma za mawasiliano anaeongoza nchini.

Charles atachukua nafasi hiyo mpya kutoka kwa Dinesh Balsingh ambae ameteuliwa kuwa Afisa Mtendaji Mkuu na Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Nigeria, kuanzia Novemba 1, 2024.

Awali, Dinesh alikuwa akitumikia nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania ambapo aliweza kuchangia mafanikio makubwa katika ukuaji wa soko la mapato ya hisa kupitia mbinu za kimkakati za masoko, ubunifu wa bidhaa na utekelezaji katika soko lenye ushindani wa hali ya juu tangu alipochukua wadhifa huo mwezi Februari 2022.

Charles Kamoto, ambae ana uzoefu wa miaka 24 katika sekta ya mawasiliano ikiwemo miaka 17 katika nafasi kubwa za uongozi – alijiunga Airtel Malawi kama Afisa Mkuu wa Biashara na baadae alianza kupanda ngazi za juu hadi kufikia nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji mwaka 2016.

Uongozi wake imekuwa na mchango mkubwa katika kufikia mafanikio ya faida, kuongeza wateja na soko la hisa ikiwemo uzinduzi wa Airtel Money Malawi kama  chapa ya huduma jumuishi za kifedha inayoongoza. Mwaka 2020, Charles alichangia kuwekwa kwa Airtel Malawi katika soko la Hisa la Malawi, na kuongeza nguvu ya uwepo wa kampuni hiyo katika ukanda huo.

Post a Comment

0 Comments