Na John Walter -Hanang'
Shirika la Development for Women and Women Trust (DWWT) limeendesha semina maalum kwa wasaidizi wa kisheria, watendaji wa kata, na Mratibu wa Ukimwi wa Wilaya ya Hanang', mkoani Manyara.
Lengo kuu la semina hiyo ni kuwawezesha washiriki kutoa elimu ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake, wasichana, na makundi ya vijana katika jamii zao kupitia Mradi wa kuimarisha na kuwezesha upatikanaji wa Haki kwa manusura wa ukatili wa kijinsia.
Akizungumza na Muungwana Blog baada ya semina hiyo, Mkurugenzi wa DWWT, Neema Khalid, alisema kuwa shirika lake limepokea msaada kutoka shirika la Women trust fund ili kupambana na ukatili wa kijinsia kupitia kuwajengea uwezo wadau wa ngazi za jamii ambao nao hufikisha elimu hiyo kwa Wanawake.
Alisema kuwa elimu kwa njia ya ushirikiano wa viongozi wa jamii ni nyenzo muhimu ya kupunguza ukatili huo kwa kuwa Wanawake wamekuwa wakipitia ukatili mbalimbali katika maeneo yao huku mabinti wakiolewa wakiwa na umri mdogo.
"Tunaamini kuwa kuwafikia viongozi hawa, hasa wasaidizi wa kisheria na watendaji wa kata, ni hatua muhimu ya kuleta mabadiliko ya kijamii" alisema Neema
Amewashauri Wanawake wanapokutana na ukatili wowote watoe taarifa kwenye ofisi za mitaa, vijiji au vitongoji na kwenye dawati la jinsia Polisi ili wapate msaada.
Amezitaja kata tatu zitakazonufaika na mradi huo ni Endasak, Gendabi, na Balangdalalu kutokana na viwango vya juu vya matukio ya ukatili wa kijinsia katika wilaya hiyo ya Hanang' na watatoa elimu kwa jamii nzima kuanzia wanafunzi, wazazi, viongozi wa dini, hadi watendaji wa serikali za mitaa.
Naye, Dominick Duncan, Mkurugenzi wa Wasaidizi wa Kisheria Wilaya ya Hanang', amelishukuru Shirika la DWWT kwa kupeleka Mradi huo katika wilaya hiyo kwa kuwa inatajwa kuwa na Matukio mengi ya Ukatili ukiwemo ukeketaji kwa watoto na Wasichana.
Amesema takwimu zinaonesha kwamba watoto wanne kati ya 10 wanakuwa wameshafanyiwa ukatili kabla ya kufikisha umri wa miaka 18.
Aidha Duncan amewataka wasaidizi wa kisheria wilaya humo kuhakikisha wanawasaidia kikamilifu waathiriwa wa vitendo vya ukatili mpaka wapate Haki zao kwenye vyombo vinavyohusika.
Washiriki wa semina wameelezea kuridhishwa kwao na mafunzo waliyopokea, wakisema kuwa yatawasaidia kuleta mabadiliko chanya katika maeneo yao.
Semina hiyo ni sehemu ya mpango wa DWWT unaolenga kuongeza uelewa wa jamii juu ya ukatili wa kijinsia na kukuza haki za wanawake na wasichana wilayani Hanang'.
0 Comments