Na John Walter- Manyara
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira inayoongozwa na Mwenyekiti Mhe. Jackson Kiswaga (Mb) imekagua miradi ya maji Hanang na kuridhishwa na utekelezaji wake.
Mhe Kiswaga amesema miradi yote iliyokaguliwa ukiwemo ule wa kurudisha huduma kwa wananchi wa Hanang' kupitia wataalam wa ndani ikisimamiwa na BAWASA, umefanyika kwa ubora na hivi sasa wananchi wanapata huduma ya maji kwa asilimia 92.
Kamati hiyo imekagua ujenzi wa chanzo cha Maji cha Mlima Hanang', ujenzi wa Mitambo ya kuchuja na kutibu maji ( Jorodom), ujenzi wa chanzo na kuunganisha maji katika Nyumba 108 zilizopo Kijiji cha Waret na mradi wa maji na Point Source Sarjanda na Kinyamburi.
Mhe. Kiswaga amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kufanikisha miradi hiyo kwa fedha.
Naibu waziri wa maji Mhandisi Mathew Kundo amesema wizara imeendelea kutekeleza miradi ya kimkakati ya kuvuta maji kutoka Ziwa Victoria na matumizi ya maji kutoka Ziwa Tanganyika huku wakitumia vyanzo vingine kama bwawa la Kidunda na bwawa la Farkwa ambalo tayari Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ameshapata zaidi ya dola 25,000 kwa ajili ya kujenga mradi huo mpaka Dodoma.
"Lakini pia tutavuta maji kutoka ziwa Victoria yakipitia Meatu, Singida mpaka Dodoma maana yake tutakuwa tumetengeneza gridi ya taifa ya maji" alisema Mahandisi Kundo
Amesema wakati mpango huo mkubwa wa muda mrefu ukisubiriwa kufanyika, serikali imeanza na uchimbaji wa visima 900 nchi nzima ili Wananchi waendelee kupata huduma ya maji.
Meneja wa RUWASA mkoa wa Manyara Mhandisi James Kionaumela amesema hadi Oktoba 24,2024 hali ya upatikanaji wa maji mjini ni asilimia 84 na vijijini asilimia 71,hivyo wastani wa upatikanaji maji kwa mkoa umeongezeka kutoka asilimia 65 kwa mwaka 2021 hadi kufika asilimia 75.5 kwa mwezi oktoba, 2024.
Mhandisi Kionaumela amesema kwa Babati mjini upatikanaji wa maji ni asilimia 98, miji midogo ya Magugu, Dareda, Bashnet na Galapo Halmashauri ya wilaya ya Babati ni asilimia ni asilimia 78.6 , Katesh asilimia, Simanjiro asilimia 97,mji wa Mbulu asilimia 66, Orkesimet asilimia 77.2 ,Kibaya asilimia 70 ambayo kwa ujumla inafanya kuwa asilimia 84 kwa mijini.
Aidha kwa Upande wa vijijini kwa kila wilaya Babati ni asilimia 80.1, Hanang' asilimia 71.1, Mbulu asilimia 69.1, Kiteto asilimia 66 na Simanjiro ni asilimia 66.7 hivyo kufanya jumla kuwa asilimia 71 kwa vijijini.
Maporomoko ya Hanang' yalisababisha miradi minne ya maji kuharibika na kuwakosesha Wananchi huduma ya maji ambapo serikali ilitoa shilingi bilioni 9 kwa ajili ya kurejesha kwenye Mpango wa kati huduma ya maji Katesh na wilaya ya Hanang' kwa ujumla ikitekelezwa na RUWASA na BAWASA.
0 Comments