Na John Walter -Manyara
Kampeni za kuwanadi na kujinadi wagombea wa nafasi za uwenyekiti wa Mitaa, vijiji na vitongoji zimezinduliwa rasmi leo Novemba 20, 2024 kwa vyama vyote vyenye wagombea Nchini.
Mkoa wa Manyara kwa chama cha Mapinduzi, kampeni hizo zimezinduliwa na Livingstone Lusinde maarufu, Kibajaji Mbunge wa Mvumi mkoani Dodoma, katika uwanja wa Motel Papa mjini Babati na kuhudhuriwa na mamia ya Wananchi na wananchama wa chama hicho.
Lusinde amewaambia Wananchi kuwa siasa sio ushabiki wa Simba na Yanga bali ni hoja , sera na msimamo na kwamba tangu kuanzishwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, chama cha Mapinduzi ndio chama bora kuliko vyote.
Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi mkoa wa Manyara Mheshimiwa Peter Toima amesema wamesimamisha wagombea kwenye mitaa 93, vijiji 445 na vitongoji 1,945 katika uchaguzi huo utakaofanyika Novemba 27 mwaka huu.
Toima amesema wamekubaliana kwa pamoja kuvunja makundi yote na kwa sasa wameungana kuwanadi viongozi wanatokana na chama hicho.
Kwa Upande wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA mkoa wa Manyara wamezindua kampeni zao katika kata ya Ayalagaya wilaya ya Babati vijijini.
Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Manyara Mathayo Gekul amesema kwenye kampeni zao watahimiza haki kwa watu kupewa wanayoyataka wakitolea mfano mfumo wa STAKABADHI GHALANI unaopingwa na baadhi ya Wakulima na wafanyabiashara mkoani humo.
Hata hivyo ameuita uchaguzi huo kuwa umenajisiwa kwa kueleza kuwa wagombea wengi wa chama chao zaidi ya 84 wameenguliwa kwenye nafasi za kugombea.
0 Comments