Hafla hiyo iliambatana na mafunzo maalum kwa wataalamu wa afya kutoka hospitali zote wilaya za mkoa wa Manyara, yenye lengo la kuboresha utoaji wa huduma kwa wagonjwa wanaosumbuliwa na magonjwa hayo yasiyo ya kuambukiza.
Akizungumza wakati wa Mafunzo hayo, Dr. John Rwegasha, Mkurugenzi wa Huduma za Tiba, Hospitali ya Taifa Muhimbili, alisema kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha huduma za afya nchini, hasa kwa wagonjwa wa magonjwa yanayohitaji matibabu ya kipekee na kwamba Kliniki hiyo itakuwa msaada mkubwa kwa jamii ya Manyara na maeneo ya jirani.
Amesema kabla ya kuanzishwa kampeni hiyo kwa ajili ya magonjwa hayo ambayo ni ya kurithi, watoto wengi walikuwa wakipoteza maisha kwa sababu ya kufanyiwa operesheni bila tatizo kujulikana hivyo kuvuja damu nyingi na kupoteza maisha na familia kukumbana na unyanyapaa.
Kwa upande wake, Dr. Lydia Barnabas, Msimamizi wa Kliniki ya Himophilia na Selimundu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara, ameishukuru wizara ya afya chini ya serikali ya Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia mafunzo hayo kwa sababu walikuwa wakipokea Wagonjwa wengi, watoto na watu wazima wanakuja na dalili, wanatokwa damu hawajui changamoto ni nini na muda mwingine wanakisia kwa kuwa hawana vipimo kugundua kwamba ni Selimundu au haemophilia.
Dr Lydia amesema vipimo na dawa vitatolewa bure kwa magonjwa hayo kuanzia sasa hadi Julai 2025 siku ya Jumannne na alhamisi kuanzia saa 2 asubuhi.
Afisa Mradi wa kuongeza Kasi ya upatikanaji huduma kwa watu wenye magonjwa ya damu Theophil Kayombo, amesema walianza tangu mwaka 2020 na wamefanikiwa kufungua Kliniki Saba awamu ya kwanza, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Mwanza, Dodoma,Kilimanjaro, Morogoro na Kigoma.
Amesema Mradi huo kwa sasa umepanga kufungua Kliniki Saba ambazo sita zitakuwa Tanzania bara na Moja Zanzibar na kote vifaa tiba na dawa za magonjwa Hayo vinapatikana kwa urahisi bila malipo.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara Sakina Kiponza, alisema kuwa uzinduzi wa kliniki hiyo ni ishara ya dhamira ya serikali katika kuboresha huduma za afya nchini na kutoa huduma zinazowalenga moja kwa moja wagonjwa wenye magonjwa maalum na kwamba watasimamia kikamilifu kupata takwimu sahihi ili kujua Hali ilivyo.
Katika kutoa ushuhuda, Mgaza Mhina, mmoja wa waathiriwa wa magonjwa ya Hemophilia na Selimundu, alieleza jinsi anavyokabiliana na changamoto za maisha na umuhimu wa huduma hizi za afya akishukuru juhudi za serikali na hospitali kwa kuhakikisha kuwa watu wanaoishi na magonjwa hayo wanapata msaada unaohitajika.
0 Comments