Na John Walter-Manyara
Katika msimu wa kilimo wa 2024/2025, Serikali imepanga kutoa ruzuku ya mbegu za mahindi zilizothibitishwa ubora kwa wakulima mkoani Manyara ili kuwapunguzia gharama kubwa za kununua mbegu hizo.
Mkuu wa mkoa wa Manyara Mheshimiwa Queen Sendiga amesema tayari rais Dkt Samia Suluhu Hassan amezindua rasmi mpango huo na kutoa miongozo na bei ya ukomo ambayo ni shilingi 14,000 kwa mfuko wa kilo mbili.
Amesema katika mbegu zilizochavushwa ambazo awali zilikuwa zikiuzwa kwa shilingi kati ya shilingi 12000-15000, sasa zitauzwa kwa shilingi 7000 kwa mfuko wa kilo mbili.
"Hayo ni mageuzi makubwa sana kutokea na kufanyika katika nchi yetu kwa sababu unapompa mkulima uhakika wa kupata mbegu bora ya mahindi unakuwa umelipa taifa uhakika wa chakula na kipato na unakuwa umeipa jamii uhakika wa maisha" alisema Sendiga
Amesema ili mkulima aweze kunufaika na mapango huo wa ruzuku ni lazima ajisajili katika mfumo wa ruzuku ambao umekuwa ukielekezwa mara kwa mara.
Mkuu wa mkoa amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kufanya maboresho katika sekta ya kilimo ili kumnufaisha mkulima.
Amemuagiza katibu tawala pamoja na katibu tawala msaidizi sehemu ya kilimo na uchumi kuhakikisha wanapunguza changamoto kubwa ya Wakulima ambao wapo maeneo ya mbali kupata mbegu hizo bora za ruzuku za mahindi.
Katibu tawala msaidizi anaesimamia uchumi na uzalishaji mkoa wa Manyara Faraja Ngerageza amesema zaidi ya Wakulima elfu thelathini (30,000) watanufaika na utekelezaji wa mpango huo wa ruzuku wa mbegu bora za mahindi.
Amesema mkoa ulinufaika na mpango wa ruzuku ya mbolea kwa kupata zaidi ya tani 13,000.
"Kilio cha watu wengi kilikuwa ni kupata ruzuku ya bei pungufu kwa ajili ya mbegu na Rais amesikia kilio hicho" alisema Ngerageza
Ni katika historia ya nchi ya Tanzania kwa mara ya kwanza kuwekwa ruzuku kwenye pembejeo za kilimo tangu uhuru.
0 Comments