NA FARIDA MANGUBE
SUA imeiomba Benki ya Dunia kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) pindi watakapoongeza fedha za maendeleo katika vyuo vikuu kuangazia maeneo yanayomilikiwa na Chuo hicho kwa kuyaboresha na kuyapa thamani kwani vyanzo vyake vya mapato vitasaidia kuongeza pato la Chuo na Taifa kwa ujumla kwa muda mfupi ujao .
Akizungumza mara baada ya kupokea ugeni kutoka Benki ya Dunia ambao ni wafadhili wa mradi huo mahususi katika kuleta Mageuzi ya Kiuchumi kupitia vyuo vikuu Tanzania, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, Prof. Raphael Chibunda amesema Mradi wa HEET umekuja wakati SUA ikitoa kipaumbele kwenye vitu ambavyo tayari vimekwisha anzishwa kwa lengo la kuviendeleza ili kuwa bora na kuleta faida.
Prof. Chibunda ameongeza kuwa, lengo la Chuo hicho si kuanza na vitu ambavyo hawakuwa navyo kabla bali ni kufanya maboresho pamoja na kutumia pesa za mradi kwenye mipango yao ikiwemo kuimarisha ufugaji wa nyuki na mazao yatokanayo na nyuki kwa kuwafundisha wanafunzi kwa vitendo hivyo ameiomba benki hiyo kuwaongezea pesa ili kujiimarisha pamoja na kuongeza thamani ya zao hilo.
Makamu Mkuu huyo ametaja eneo lingine lenye tija ni Olmotonyi Arusha lenye mazao ya misitu yanayochakatwa ambapo mwaka jana kwa pesa za ndani Chuo hicho kilinunua mashine ya uchakataji hivyo kupitia mradi huo wataweza kutanua na kuuza bidhaa zenye thamani ya juu pamoja na kuwafundisha wanafunzi jinsi ya kufanya vizuri zaidi.
Aidha amesema Chuo kilikuwa na mkakati wa kupunguza utegemezi wa fedha za Serikali wakanunua ardhi ya hekari 10,000 mkoani Ruvuma ikiwa ni mpango wao wa kuendelea kupanda miti na kwamba kama watapata ongezeko la fedha wataweza kumalizia kupanda katika eneo lingine lilipo kilometa kumi kutoka eneo walipopanda awali hivyo kwa miaka 5 ijayo chuo kitaweza kupata mapato kupitia misitu yake ikiwa pamoja na bishara ya hewa ukaa.
“Kama unataka kusaidia Afrika kubadilika kuna uhitaji wa kuwaelimisha watu wake hivyo SUA tunayo mashamba darasa ambayo yanazalisha mazao mbalimbali yanayotumika kwa mafunzo pia kibiashara hivyo endapo Mradi wa HEET utatusaidia kufikia malengo tutanunua eneo kwa ajili ya kufugia samaki, shamba la maziwa ndani ya miaka 20 kutakuwa na mabadiliko makubwa chuoni”. Amesema Prof. Chibunda
Naye Kiongozi wa Timu ya Benki ya Dunia Prof. Roberta Maree amekipongeza Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kwa kuwa na mikakati endelevu iliyokwishaanza kufanyika kwani wao kama benki ya dunia wanaangalia Taasisi ama vyuo vyenye kuleta mabadiliko kiuchumi ili kuwasaidia kuendelea kufanya kwa ufanisi zaidi pasi kuwekeza katika mawazo ambayo hayajaanza kufanyiwa kazi.
Aidha Prof. Maree amesema SUA ni Taasisi ya kipekee imeshirikiana na Benki ya Dunia huku ikiendelea kufanya vizuri upande wa Elimu na Tafiti, wanatambua malengo na nia Chuo hicho katika kufanikiwa kupitia benki ya dunia kwa kuwa wanayo sifa ambayo wao wanaitaka hivyo amewataka waendelee kushirikiana ili kuleta mageuzi ya kiuchumi nchini.
0 Comments