Na John Walter -Babati
Mkuu wa Wilaya ya Babati, Emmanuela Kaganda, ameonyesha kutoridhishwa na baadhi ya taasisi kutokushiriki sherehe za miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania, zilizofanyika leo Desemba 9,2024.
Katika hotuba yake akifungua mdahalo maalum kuhusu uhuru, Kaganda alieleza kuwa kitendo cha taasisi hizo kutoonekana katika sherehe hizo ni dhihirisho la ukosefu wa uzalendo na kushindwa kutambua umuhimu wa siku hiyo adhimu kwa Taifa.
Akizungumza kwa msisitizo, Kaganda aliagiza taasisi zote ambazo hazikuhudhuria sherehe hizo kuwasilisha maelezo ya maandishi yakieleza sababu za kutokushiriki.
Aliongeza kuwa hatua hiyo ni muhimu ili kuhakikisha kila taasisi inawajibika ipasavyo na inatoa mchango wake katika matukio ya kitaifa yanayojenga mshikamano na heshima kwa nchi.
“Sherehe za Uhuru siyo tu siku ya kumbukumbu, bali ni fursa ya kuonyesha mshikamano wetu kama Taifa, Kutohudhuria ni sawa na kudharau historia ya nchi yetu na juhudi za waasisi wa Uhuru" alisema Kaganda
Tunahitaji kujua sababu za kushindwa kwenu kufika, ninaomba mdahalo huu urudiwe wakihusishwa Vijana, Wanafunzi na taasisi zote" alisema Kaganda
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya alisisitiza umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika matukio ya kitaifa kama njia ya kudumisha mshikamano wa kijamii na uzalendo miongoni mwa Watanzania.
Miaka 63 ya uhuru wa Tanzania unaadhimishwa leo kwa ngazi za mikoa na wilaya ili kuwakumbusha wananchi wapi nchi imetoka, ambapo katika mkoa wa Manyara imefanyika mjini Babati ikiongozwa na mkuu wa wilaya ya Babati kwa niaba ya mkuu wa mkoa Mheshimiwa Queen Sendiga.
0 Comments