F Mama wa Miaka 44 Afariki Baada ya Kuumwa na Nyoka, Tuhuma za Uzembe Zaibuliwa | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Mama wa Miaka 44 Afariki Baada ya Kuumwa na Nyoka, Tuhuma za Uzembe Zaibuliwa


Na John Walter -Babati 

Juliana Obed, mwanamke mwenye umri wa miaka 44 kutoka kijiji cha Magugu, wilayani Babati, mkoani Manyara, amefariki dunia baada ya kuumwa na nyoka.

Tukio hilo limetokea  mnamo tarehe 15 Desemba 2024 majira ya saa 11 jioni wakati alipokuwa akichuma mboga nje ya jengo la kanisa la Magugu, ambalo mume wake alikuwa akilipaua.

Kwa mujibu wa mume wa marehemu, Obed Laizer, baada ya tukio hilo alimkimbiza mke wake katika Kituo cha Afya cha Magugu kwa ajili ya matibabu,Hata hivyo, alidai kuwa madaktari kituoni hapo walikataa kumtibu mgonjwa bila kulipwa kwanza kiasi cha shilingi laki moja na nusu (150,000).

Obed anasema licha ya yeye kukubali kulipa kiasi hicho, madaktari waligoma kuanza matibabu hadi pale walipoona fedha hizo mkononi,Kutokana na ucheleweshaji huo, hali ya mgonjwa ilizidi kuwa mbaya na hatimaye akapoteza maisha akiwa kituoni hapo majira ya saa 12 jioni.

Tukio hilo limeibua hasira miongoni mwa wakazi wa kijiji cha Magugu, ambao wamelalamikia uzembe wa madaktari katika kutekeleza majukumu yao huku wakitoa wito kwa serikali kuboresha huduma za afya ili kuzuia matukio kama haya kutokea tena.

Mwenyekiti wa kijiji cha Magugu Lohay Amos ameahidi kufanya uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo na kusema hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wahusika endapo itabainika uzembe huo ulisababisha kifo cha marehemu.

Marehemu Juliana Obed ameacha mume na watoto watano.


Post a Comment

0 Comments