Na John Walter -Babati
Mkuu wa Wilaya ya Babati Mhe. Emanuella Kaganda amewaongoza Wananchi na Watumishi wa Wilaya ya Babati kuadhimisha miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania kwa kupanda miti na kuwatembelea wagonjwa hospitali ya mji wa Babati (MRARA).
Maadhimisho hayo yamebeba kauli mbiu isemayo "Uongozi Madhubuti na Ushirikishwaji wa Wananchi ni Msingi wa Maendeleo yetu"
Katika hotuba yake Mhe. Kaganda amewaeleza Wananchi kuwa siku ya tarehe 9 Desemba ni siku muhimu kwa Taifa la Tanzania kwa kuwa Hayati Baba wa Taifa Mwl.Julius K. Nyerere na Viongozi wengine walifanya kazi kubwa kutufikisha katika Maendeleo ya sasa.
Aidha Kaganda amewataka Wananchi kuwaombea wapigania Uhuru na kufanya kazi kwa bidii ili kuijenga Tanzania ya kesho.
Shughuli mbalimbali zilizofanyika ni pamoja kufanya mazoezi kuimarisha afya kwa na kufanya matembezi (jogging), kupanda miti ya matunda na vivuli katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji Babati (Mrara)pamoja na kutoa zawadi kwa wazazi na wajawazito.
Sambamba na hilo katika mdahalo, Wananchi na Wazee wameeleza kuwa Tanzania imepata Maendeleo makubwa yakiwemo, uboreshwaji wa huduma za afya, uboreshwaji wa miundo mbinu ya Barabara, Maendeleo ya viwanda na Biashara , Maendeleo ya makazi, Maendeleo ya elimu Sayansi na Teknolojia pamoja na uwezeshwaji wa kiuchumi kwa Wananchi wakiwemo Vijana kupitia mikopo ya asilimia 10% ya halmashauri.
"Kwa kipindi Cha nyuma tulikuwa tunatumia siku tatu hadi tano kusafiri lakini kwa sasa Miundombinu imeboreshwa tunatumia siku moja" ameeleza Bi. Masiweta Sanka.
Sanka aliwahimiza vijana kuwa wazalendo kwa Nchi yao, kufanya kazi kwa bidii na kuwa mstari wa mbele kukemea vitendo vya rushwa.
0 Comments